Mbunge Kinondoni ajiunga rasmi na CCM
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/12/mbunge-kinondoni-ajiunga-rasmi-na-ccm.html
Mbunge wa Kinondoni jijini Dar, Maulid Mtulia (CUF) leo ametangaza kujiuzulu ubunge na kujivua uanachama wa Chama cha Wananchi CUF na kuhamia CCM.
Katika barua yake ya kujiuzulu, Mtulia amesema kuwa ameamua kufanya uamuzi huo leo Disemba 2, kwa utashi wake bila shinikizo la mtu yeyote.
Mtulia ameelezea sababu za kujiuzulu nafasi yake hiyo ya ubunge na kuhama chama kuwa imetokana na uzoefu alioupata kwa miaka miwili ya ubunge, na kusema “nimebaini kuwa Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ni chama tawala inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo sisi upinzani tuliahidi kuyatekeleza” alisema.
Aidha Mbunge huyo amesema kuwa nia yake ni kuwatumikia wananchi, na haoni sababu ya kuendelea kuwa upinzani na badala yake anaona ni vema aungane na juhudi za Serikali, kwa kumuunga mkono Rais Dk. John Magufuli katika kuwaletea wananchi maendeleo na kukabiliana na kero mbalimbali.
Mtulia amesema anawashukuru wananchi wa Jimbo la Kinondoni, kwa kumpa dhamana ya ubunge, katika uchaguzi mkuu uliopita na amewaahidi kuwa yupo tayari kuendelea kushirikiana nao katika maendeleo, akiwa katika uwanja mwingine wa siasa ambao ni Chama Cha Mapinduzi.