Wakurugenzi waagizwa kupima maeneo ya Shule kuepuka migogoro
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/wakurugenzi-waagizwa-kupima-maeneo-ya.html
NA MWANDISHI WETU,TABORA
WAKURUGENZI Watendaji wameagiza kuhakikisha maeneo ya
Shule na Taasisi nyingine za elimu yanapimwa haraka na kuwekewa mipaka ili
kuepuka uvamimizi unaofanywa na watu na kusababisha migogoro ambayo imekuwa
ikichelewesha maendeleo.
Kauli hiyo imetolewa
hivi karibuni mkoani Tabora na Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais ,
Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa( TAMISEMI ) Tixon Nzunda wakati
akizungumza na Watendaji na watumishi wa Mkoa huo.
Alisema kuwa hatua hiyo
itasaidia kuondoa migogoro kati ya uongozi wa Shule husika na wavamizi wa
maeneo hayo.
Nzunda alisema kuwa
migogoro inayotokana na uvamizi wa maeneo ya shule imekuwa ikiathiri maendeleo
ya wanafunzi na taaluma kwa sababu uongozi wa shule wakati mwingine umekuwa
ukishindwa kupanua miundo mbinu kwa ajili ya utoaji wa elimu kwa wanafunzi.
Alisema kuwa ili kuepuka
tatizo hilo kuendelea kujitokeza katika maeneo mbalimbali ya shule ni kwa
Wakurugenzi Watendaji kwa kushirikiana na watendaji wengine kama vile watu wa
mipango miji kuhakiki maeneo yote yanamilikiwa na Shule na kuwaondoa ambao
wameingia.
Aidha Naibu Katibu Mkuu
huyo aliwaagiza Wakuu wote wa Shule kuhakikisha kuwa maeneo yao yanapandwa miti
mipakani na maeneo mengine ya shule ikiwa ni hatua ya kukabiliana na uvamizi
unaofanywa na watu wanaoingia baada ya kuona maeneo hajafanyiwa uendeleza
wowote.
Aliongeza kuwa pia
wanatakiwa kupanda maeneo ya shule maua ikiwa ni sehemu ya kufanya mazingira
yavutie wanafunzi kwenda kujifunza.
Katika hatua nyingine
Naibu Katibu Mkuu huyo amewaagiza walimu kuhimiza pia masomo ya michezo na
Sanaa mashuleni ikiwa ni sehemu ya kuwavutia wanafunzi wengi
kuhudhuria shuleni.
Alisema kuwa ni vema
wakatumia fedha kidogo wanayopata kununulia vifaa vya michezo na Sanaa ili
kuwapa fursa wanafunzi kuonyesha vipaji vyao mapema ambavyo vinaweza kuwasaidia
katika maisha yao ya baadaye kama vitaandaliwa na kulelewa vizuri toka awali.
Nzunda alisisitiza kuwa
michezo na Sanaa ni sekta ambazo zimesaidia vijana kujiari sehemu
mbalimbali duniani , hivyo ni vema walimu wasaidie kuwaandaa wanafunzi ili
waweze kushiriki kikamilifu katika eneo hilo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji
wa Manispaa ya Tabora Bosco Nduguru alisema kuwa kwa upande wao wameshaanza
kuwaondoa wavamizi wa maeneo ya Shule ambapo hivi karibuni waliowaondoa
wavamizi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Tabora kwa kuvunja nyumba
zilizojengwa katika eneo hilo.
Alisema kuwa wanataraji
kuwaondoa wakati wowote waliovamia maeneo mengine ya Shule kama wale wa Shule
ya Sekondari MIlambo na kwingineko na kisha kuweka uzio.