Ujenzi Magomeni Kota Kukamilika Machi Mwakani
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/ujenzi-magomeni-kota-kukamilika-machi.html
NAIBU Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Mheshimiwa Elias Kwandikwa (Mb), ameutaka Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA), kufanya kazi kwa bidii katika miradi yote inayopewa na
Serikali ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.
Akikagua hatua
zilizofikiwa katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni kota, Kwandikwa,
amesema Serikali itaendelea kuainisha miradi mingine ili kuhakikisha fedha za
Serikali zinaokolewa na kusimamiwa kwa uzalendo.
“Hakikisheni
mnafanya kazi zenu kwa weledi, uzalendo na kukamilisha miradi kwa wakati na
kuokoa fedha ambazo zitatumika katika utekelezaji wa miradi mingine hapa
nchini”, amesisitiza Mhe. Kwandikwa.
Muonekano wa mtambo wa kuchakata zege unaotumiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota, jijini Dar es Salaam. |
Ametoa wito kwa
wataalamu wengine kuja kupata mafunzo kwa TBA ambao ni chachu ya utekelezaji wa
miradi mingi hapa nchini kwa kuwa wanatumia mfumo wa kisayansi na mitambo yenye
kusaidia kupunguza gharama za ujenzi.
Pia, Naibu
Waziri huyo ameushukuru uongozi wa TBA kwa kutoa ajira za vibarua takribani 200
kwa siku katika mradi huo na kuwataka wafanyakazi hao kuwa waadilifu na waaminifu
ili kuwa na sifa za kupata ajira za kudumu.
Muonekano wa baadhi ya vitalu vya makazi eneo la Magomeni Kota zinazojengwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 35. |
Naye Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Majengo Tanzania (TBA), Msanifu Majengo Elius Mwakalinga, amemhakikishia Naibu
Waziri Kwandikwa kukamilika mradi huo kwa wakati, ubora na kwa gharama nafuu.
Amefafanua
kuwa mradi huo utakuwa una jumla ya vitalu vitano ambapo vitalu vinne vina
majengo ya ghorofa nane na kitalu kimoja kina jengo la ghorofa tisa na hivyo
mradi utatoa makazi kwa kaya 656.
Mradi wa
ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Magomeni Kota unatarajiwa kukamilika ifikapo
mwezi Machi mwakani na utagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 20 zote ikiwa ni
fedha za Serikali.