UVCCM na kampeni Sambaza Bendera, kugusa kitasa cha Tanzania ya Viwanda
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/uvccm-na-kampeni-sambaza-bendera-kugusa.html
NUKTA ya kwanza ya dhamira ya nembo ya Jumuiya ya
Vijana wa Chama cha Mapinduzi
(UVCCM) ni kuleta matumaini pasipokuwa
na matumaini hayo.
Wakati nukta ya pili, nembo hiyo inawataka vijana hao
kuhamasisha upendo pale penye chuki.
Kwamba thamani ya binadamu ni kujaliani,
kuhurumiana, kusaidiana katika hali zote.
Vilevile kushirikiana katika uzalishaji
mali na kugawana pato la taifa kwa njia huru, haki na usawa kwa vile kila mtu
anastahili heshima, kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake.
UVCCM Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam umekuja na mpango wa Siasa
ni Uchumi unaoakisi nukta ya tatu ya dhamira ya nembo hiyo inayowataka vijana
kujenga taifa kwa kufanya kazi kwa bidii kwa njia ya vikundi vya kisiasa kwa
msingi kwamba, kazi ndio msingi wa heshima
kwa binadamu yeyote mwenye nguvu na akili timamu.
Katibu wa Umoja huo Wilaya ya Kinondoni, Rashidi
Semindu Pawa anasema mpango wa Siasa ni Uchumi unatekelezwa kupitia programu ya
uwekaji wa bendera kwenye maeneo yote ya CCM wilayani humo sambamba na kufungua
mashina mengi ya wakereketwa wa umoja huo kwa lengo la kusogeza huduma karibu
na wanachama na jamii kwa ujumla.
Hiyo ni pamoja na kuanzisha shughuli za uzalishaji
mali, biashara, kushiriki shughuli za kijamii na kitaifa za kiserikali, chama kama ilivyoanishwa kwenye
malengo ya kuanzishwa kwa Umoja wa Vijana wa CCM tangu wakati wa TANU Youth
League (TYL) miaka ya 1950’s.
Anasema
mpango wa usimikaji wa bendera za CCM umezinduliwa kwa mara ya kwanza katika
historia ya UVCCM wilaya ya Kinondoni katika tawi la Makongo Kati, Kata ya Makongo Oktoba
22 mwaka huu na kusema kuwa lengo ni kufika Kata zote 20 za CCM Wilaya ya Kinondoni huku akiupongeza uongozi wa tawi hilo kuwa wa
kwanza katika ubunifu wa mpango hu.
“Tuna uasisi hapa Tawi la Makongo, lakini tutahakikisha kwamba
tunaupeleka kila kata na tawi kwa vile malengo yake yana tija kisiasa na
kiuchumi…huu ni mpango muhimu kwa kundi la vijana ambao ni muhimu kufanya
shughuli kwa vikundi au umoja hasa wakati huu taifa likiwahitaji kwa ajili ya
kufikia malengo ya ilani yetu ya uchaguzi ya mwaka 2015 na sera ya CCM ya taifa
la uchumi wa kati kwa njia ya viwanda kwa kufanya kazi,”anasema Semindu.
Katibu huyo wa UVCCM wa Wilaya ya Kindondoni anasema
ili kufikia malengo hayo ni lazima vijana kujiunga kwenye mpango huo, ambapo
kupitia shughuli za kisiasa na biashara ni rahisi kutambulika na kuwa wa kwanza
kuingizwa kwenye mipango ya serikali hasa mikopo, kwa kuwa Mpango wa Serikali wa
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi unalenga makundi yaliyoanzishwa na kusajiliwa
badala ya mtu mmoja mmoja.
“Nawapongeza Tawi la Makongo Kati kwa kuanzisha
programu hii muhimu, sasa naagiza Makatibu wote wa Matawi na Kata wa Umoja wa Vijana
Wilaya ya Kinondoni kuiga mfano huu,
nasisi Wilayani tunauchukua kuwa mpango
wa Wilaya nzima,”alisema.
Anasema lengo kuu la mpango huo ni kuongeza idadi ya
wanachama wa Umoja huo na CCM, kuimarisha, kuongeza imani na itikadi ya CCM
ambazo shughuli hizo zinaweza kuwafanya na watu wengine wasiokuwa na itikadi
hiyo kujiunga na wale walioingia na kufanya shughuli za kisiasa kwa mfumo wa
kiuchumi.
Ili kufikia vijana kufikia malengo wanayoyaweka,
amewaasa kuwa wavumilivu, msimamo hasa wa itikadi ya CCM kwa vile ndiye yenye serikali ambayo
inamiliki uchumi na fedha za uma na kuwa rahisi kwao kukopeshwa na sio
vinginevyo.
Pia aliwaasa kuzingatia nidhamu, uhusiano bora, kufanya
kazi kwa bidii na kuwa watu wenye msimamo katika maisha yao yotea na kusema mambo hayo ni muhimu katika kumjengea heshima mtu
mahali popote.
Suzan Godfrey Byemelwa ni Mwenyekiti wa Umoja huo
Tawi la Makongo Kati, ambalo ni waasisi wa mpango wa kupandisha bendera chini
ya kauli mbiu yao iitwayo `Kutafuta
Kilichopotea, Siasa na Uchumi’
anasema madhumuni ya tawi lake kuja na mpango huo ni kuhamasisha kampeni
ya kuongeza wanachama kupitia shughuli za ujasiriamali kwenye mashina na
hatimaye kila kijana kushiriki kikamilifu katika kufanya kazi.
Pia inalenga kufanya shughuli zingine za uzalishaji
mali kwa njia ya kilimo, ushonaji wa nguo, ufugaji , michezo na kushirikiana na watu katika jamii
katika kuhamasisha utekelezwaji wa ilani ya CCM kwa vitendo hasa kwa kuanzisha
viwanda vidogo vidogo vya uchakataji wa mazao ya kilimo na ufugaji kama muhogo
na mazao ya samaki na mifugo.
“Tuna dhamira na suala hili la kutaka tufanye siasa
kisayansi…utafiti wetu kwa kushirikiana
na viongozi wetu wakuu wa chama Tawini Chini ya Kamati Siasa ya Tawi
tumebaini kwamba matumizi ya nguvu kazi ya vijana hapa nchini hayajakidhi
matakwa ya Dira ya Maendeleo ya Taifa na Mpango wa Maendeleo ya Milenia (MDGs)
katika kupunguza na kutokomeza umasikini kwa kutumia fursa zilizopo,”anasema.
Anasema kati ya vijana wa CCM 100 waliohojiwa kuhusu
ushiriki wao katika Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umasikini
(MKUKUTA), Mkurabita na Mkumbita, zaidi
ya asilimia 60 hawafahamu mipango hiyo jambo ambalo ni rahisi kurubuniwa na
kukosa msimamo kisiasa na kiuchumi.
Anasema ili kufikia malengo hayo umoja huo wao umjiwekea
mpango kazi wa miaka mitano katika kipindi cha 2017 hadi 2022 kutafuta shamba
nje ya Dar es Salaam na kushiriki katika shughuli za pamoja za kilimo ambazo
zitazidi kuwaunganisha vijana na kufanya siasa inayoaminika kutokana na uhakika
wa kipato kutokana na shughuli hizo.
“Kwa sasa tunayo biashara ya kuuza mkaa katika shina
letu la wakereketwa namba 2, lakini malengo yetu sio kuendelea na biashara hii
inayochochea uharibifu wa mazingira wakati katika mipango yetu ni kuwa na mradi
wa bustani ya miti kibiashara kwa nia ya kupambana na madiliko ya tabia nchi
kwa kupanda miti kwenye maeneo mbalimbali,”anasema.
Anasema baada ya kufanikiasha hatua hiyo,
wanakusidiwa kuwasilisha andiko la mradi wa kilimo katika Benki ya Maendeleo ya
Kilimo (TADB) na Benki ya Maendeleo ya Vijana ili ikiwezekana benki hizo
zisaidie juhudi na mtaji wao.
Katibu wa CCM Kata ya Makongo, John Makata anasema
mpango wa usimikaji wa bendera ni jambo mtambuka kutokana na umuhimu wake
kisiasa, kiuchumi na kijamii na kusema CCM katika Kata hiyo kinatoa baraka
kwenye matawi yote ya CCM kusaidiana na
Jumuiya za Vijana katika kuutekeleza.
Kamata
anasema shughuli za kiuchumi ni muhimu katika kufanya siasa endelevu kutokana
na tatizo la umasikini kuwa chanzo kikuu cha wanasiasa wenye hasa kundi la
vijana kutokuwa na msimamo wa maisha na kiitikadi.
Pia ni lazima kutolewa kwa mafunzo endelevu ya
shughuli za uzalishaji mali kwa njia ya ujasiriamali ili metholojia hizo ziweze
kujengeka katika akili miongoni mwa vijana ili kuondokana na hali tegemezi,
ombaomba na itikadi isiyoeleweka.
“Tunapozungumzia suala la usaliti wakati
mwingine husababisha na hali duni ya maisha, kama wanachama wetu
hawatafundishwa mbinu za kujikwamua kiuchumi
na kuwezeshwa, ni wazi kwamba ni vigumu sana kutokomeza adui usaliti
ndani ya chama chetu pasipo uwekezaji wa methodolojia za kisiasa hasa itikadi
sahihi na shughuli za kiuchumi,”anasema.
Kwa
mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012
katika kila watu 10 wa Tanzania, wanne ni vijana ambao umri wao ni
kati ya miaka 15 na 35. Idadi ya kundi hilo ni asilimia 35 sawa na milioni 16.
Mkoa wa Dar es Salaam una asilimia kubwa zaidi ya vijana huku Singida ikiwa na
asilimia ndogo zaidi ya watu walio katika kundi hilo.
Pia
asilimia 52.2 ya watu nchini wana umri wa kufanya kazi ambao ni kati ya miaka
15 na 64, huku ikielezwa kuwa rasilimali watu kwa ajili ya kuzalisha na
kuongeza uchumi na kupunguza umasikini hapa nchini si tatizo kinachotakiwa ni watu kutumia fursa
zilizopo kufanya kazi kwa bidii ili kuinua uchumi.
Alitaja mkoa unaoongoza kwa kuwa na watu wengi
wa kufanya kazi ni Dar es Salaam ambako kwa kila watu watatu, wawili wana
umri wa kufanya kazi huku Simiyu ikiwa na idadi ndogo ambayo ni asilimia
45.5.
Takwimu hizo zimebainisha kuwa idadi ya watu wenye umri wa miaka 60 na zaidi ambao ni wazee ni milioni 2.5 sawa na asilimia 5.6 ambapo mkoa unaoongoza kwa kuwa na wazee wengi ukiwa Kilimanjaro ambao una asilimia 9.7 , Dar es Salaam ikiwa na wazee wachache sawa na asilimia 3.5.
JIUNGE
NASI , BONYEZA
HAPA http://www.raiatanzania.blogspot.com ku-install App ya
raiatanzania, bila
ya kuingia website Tweet@Raia
Tanzania online, youtube@Raia Tanzania online TV, Fb@Raia Tanzania online,
insta@raia Tanzania online