Mbunge CCM awapasha polisi, wakuu wa mikoa
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/mbunge-ccm-awapasha-polisi-wakuu-wa.html
KATIKA siku za hivi
karibuni kumekuwa na malalamiko juu ya utendaji wa Jeshi la Polisi, wakuu wa
mikoa na wakuu wa wilaya kuhusiana na kutozingatia sheria na utaratibu katika
utekelezaji wa majukumu yao.
Katika makala haya,
Raia Tanzania limefanya mahojiano na Mbunge wa Kavuu (CCM), Dk. Pudenciana
Kikwembe, ambaye pamoja na mambo mengine kuhusu jimbo lake, anaelezea
changamoto zinazosababishwa na hali hiyo.
Raia Tanzania: Umekuwa kwenye siasa kwa misimu mitatu hadi
hivi sasa tangu ulipoingia bungeni mwaka 2005 ulipogombea ubunge wa viti
maalumu katika mkoa wa Rukwa, je hali ya siasa kwa sasa unaionaje ukilinganisha
na mwaka ambao ulianza kijihusisha na mambo haya?
Dk. Kikwembe: Siwezi kusema moja kwa moja kuwa ni
mbaya ama nzuri na uzuri wake au ubaya wake kwa sababu inataegemea
imemgusa nani na kwa wakati gani.
Lakini naweza kusema
kwamba kwa namna nyingine sio nzuri kutokana na mamlaka ambayo Jeshi la Polisi
limepewa hivi sasa. Jeshi la Polisi lipo kwa ajili ya kulinda usalama wa raia
na mali zao na kweli linatimiza wajibu wao kama inavyotakiwa, lakini huku
kwenye mambo ya saisa elimu zaidi inahitajika wapewe.
Wananchi bado
hawajapata elimu ya kutosha kuhusu masuala ya kisiasa, misingi ya kidemokrasia,
mfano amri za wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya namna ambavyo wanavyotumia Jeshi
la Polisi kuvunja amani ya wananchi.
Wakati mwingine amri
zao zinaweza kusababisha hali ya uvunjifu wa amani ambayo tunayo Watanzania.
Jeshi la polisi limekuwa likileta shida kwenye majimbo na tatizo hilo linatokana na amri za wakuu wa
mikoa na wilaya.
Mbunge anatangaza kuwa
atakuwa na mkutano na wananchi jimboni kwakwe na hilo jambo halijakatazwa, kila
Mbunge ameruhusiwa kufanya mkutano kwenye jimbo lake, lakini unakuta polisi
wanafika pale na kuanza vurugu, wanasema hakuna mkusanyiko, sasa wananchi
wanachanganyikiwa hawajui wamsikilize nani. Polisi wanatakiwa watumie kanuni na
sheria zao kwa umakini, elimu kwanza itolewe kwa polisi ili waweze kufanya kazi
vizuri na wanasiasa kuliko hivi sasa ambavyo wanafanya.
Pia kuwepo na
ushirikiano kati ya Mbunge, mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya, kusiwepo na
mikinzano kwamba huyo ametoa agizo hili na yule nae ametoa agizo hili, tufanye
kazi kwa pamoja.
Raia Tanzania: Hili la Jeshi la Polisi kuzuia mikutano
ya hadhara unazani limewaathiri vipi kama wanasiasa?.
Dk. Kikwembe: Mikutano ya hadhara sidhani kama
imezuiliwa, ila ninachofahamu kilichozuiliwa ni maandamano ambayo hata mimi pia
siyaungi mkono.
Wabunge tunafanya
mikutano kwenye majimbo yetu na huu ni utaratibu mzuri na kikubwa hapa hakuna
athari yoyote kwa sababu kama mbunge anafanya mkutano na wananchi wake huko ni
kujijenga.
Tunapozungumzia
kujijenga kisiasa sio lazima mfanye maandamano, ninamna ambavyo tu
wanasiasa wengine wanavyolichukulia jambo hili kana kwamba linatupoteza
lakini sio kweli, kikubwa ni watu wafuate sheria na kanuni ambazo
zimewekwa.
Raia
Tanzania: Unazungumziaje hali ya usalama kwa wabunge, kumekuwa
na matukio kadhaa wabunge wana lalamika kuhusu usalama wao, je kwa upande wako
ikoje?.
Dk.
Kikwembe: Jambo hili kwakweli
limefanya kila mmoja amekuwa na hofu, kila mmoja anapigania uhai wake, usalama
kwa wabunge umekuwa mdogo sana, ndio mana wabunge tumeomba kupewa ulinzi.
Hapo awali watu
walikuwa salama, hakukuwa na matukio kama ambavyo tunaona hivi sasa.
Jambo hili limeleta
mshangao kwa kila mmoja, jambo ambalo limefanya kila mmoja kuwa na hofu, wenyewe
kwa wenyewe hivi sasa hatuaminiani kabisa, unakuwa ndani ya bunge ikifika muda
wa kutoka unawaza kuvamiwa, kikubwa wabunge tujitahidi kuchukua tahadhari sisi
wenyewe.
Raia Tanzania: Unazungumziaje hili la wabunge kukamatwa
hovyo.
Dk. Kikwembe: Kinga ya mbunge ipo ndani ya bunge, lakini
wakati mwingine mambo hayo ya kukamatwa yanatokana na matamko ambayo wanayatoa
kwenye maeneo wanapokuwa.
Kama mbunge
unaposimama kwenye jukwaa kuzungumza na wananchi wako lazima uangalie maneno ya
kuzungumza, sio kila neno unatakiwa kulisema, wakati mwingine haya mambo lazima
ifikie hatua tujitafakari mwenyewe kabla ya kuzungumza.
Unakuta mbunge anazungumza
na vyombo vya habari ama mkutano anatoa matamko makali hadi
unajiuliza hivi huyu alikuwa na maana gani, kwanini anazungumza hivi, hata kama
ni kutafuta umarufu sio kwa namna hii.
Raia Tanzania: Kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wabunge wa
vyama vya upinzani kuwa wabunge wa CCM mmekuwa mkipitisha vitu kwa masilahi ya
chama na sio taifa, pengine hili likoje ikiwa wewe ni mbunge wa chama tawala?.
Dk.
Kikwembe: Tunapokuwa tunapitisha
jambo lolote kwa pamoja ni kutokana na kuwa tayari lilishajadiliwa na
kupitishwa kwenye kamati zetu za kibunge, ambapo huko tupo wabunge wa vyama
vyote.
Lakini pia ieleweke
kuwa CCM ndio kipo madarakani hivi sasa, hata wao ikija kutokea kuwa chama chao
ndio kinaongoza nchini lazima wapitishe kwa ajili ya kuunga mkono chama chao.
Ila kinachotokea ni
kwamba tunapokuwa bungeni tunataka kupitisha vitu kama bunge na sio kamati
zinakuja changamoto za kiitikadi ya vyama.
Lakini pia wakati
mwingine ipo miswaada ambayo inaletwa bungeni kwa ajili ya kupitishwa kama
bunge kwa dharura na hapo kama bunge linatakiwa kufanya maamuzi ya haraka
lakini sio kwamba wabunge wa CCM tunafanya mambo kwa ajili ya chama
.
Raia Tanzania: Kuna msemo ambao ni maarufu sana kwa wanasiasa
ambapo pia umeambukizwa hadi kwa wananchi: “Tunaisoma namba” hii kauli ikoje?.
Dk. Kikwembe: Kweli haya mambo yapo, kauli ya kuisoma
namba ina maanisha maisha magumu, Rais wetu Dk. John Magufuli anataka wote
tulingane kusiwe na matabaka ya wenye nacho na wasio nacho, lazima wote tuwe
sawa.
Raia Tanzania: Tunaona upande wa pili wa wabunge wa upinzani
wamekuwa wakilalamika kuwa wabunge wa CCM wanafanya mikutano bila kupata
bugudha kutoka kwa Jeshi la Polisi lakini inapotokea kwa upinzani kamata kamata
zinakuwa nyingi, ukiwa mbunge unayetokana na chama tawala unazungumziaje kauli
hiyo?
Dk. Kikwembe: Hili jambo sio kwamba upinzani wanaonewa
kukamatwa na polisi na wala sio wao peke yao ambao wanakamatwa, hii inatokana
na kutokufuata utaratibu.
Ukiangalia suala la kukamatwa sio wapinzani peke yao,
hivi karibuni alikamatwa Mbunge wa Hanang Dk. Mary Nagu, huyu ni mbunge ambaye
anatokana na CCM, kwahiyo hakuna ambaye anaonewa tuna rudi kulekule kuwa kila
mmoja afuate sheria.
Raia Tanzania: Nichangamoto zipi ambazo unakutana nazo
katika jimbo lako?
Dk.
Kikwembe: Changamoto ni nyingi
hususan za kimaendeleo, kama vile maji, umeme na barabara, hadi sasa nimepeleka
visima 18 vya maji ambavyo vimeanza kuchimbwa.
Suala la madarasa na
madawati wananchi wanachangia nashukuru kwamba wana mwitikio katika uchangiaji
wa shughuli za maendeleo, nipo karibu na wananchi wangu katika kutatua
changamoto zilizopo.
Katika kukabiliana na
tatizo la maji na shukuru Rais Dk. Magufuli kuanzisha kampeni ya kumtua
mama ndoo kichwani.
Lakini pia katika
kampeni za uchaguzi aliahidi kila kijiji Sh. milioni 50, nitumie nafasi hii
kuwaambia wananchi wangu kuwa fedha hizo zipo na kwa sasa serikali inaandaa
utaratibu wa kuzileta fedha.
Raia Tanzania: Kwa uzoefu ulionao, unazungumziaje uelewa wa
wananchi kwenye majimbo ambayo mnatoka, lakini pia wananchi wanaelewa nini
kuhusu siasa?
Dk. Kikwembe: Ninachokifahamu hadi sasa wananchi wengi
wanatambua kuwa siasa ni uchaguzi, hata wanasiasa wengine ambao hawapo
madarakani wanafahamu hivyo, ndio maana hivi sasa unaona wapo ambao wanapita
kwenye majimbo kutafuta kura.
Ukiangalia hivi sasa
majimboni kumeanza mchezo mchafu wa kwenda kutafuta kura kabla ya muda wake
kufika, ninachofahamu ni kwamba watu wanapomaliza uchaguzi mkuu mbunge
aliyechaguliwa anakuwa na kazi ya kuwatumikia wananchi wake ndani ya jimbo na
nje ya jimbo kwa maana akiwa bungeni.
Lakini sasa
kinachotokea ni kwamba mbunge akiwa bungeni huku nyumba kuna mtu anamvizia kuwa
akitoka nitaenda kuzungumza na wananchi ili wamchague na ukizingatia wananchi
wanafahamu kuwa siasa ni uchaguzi sio maendeleo.
Ukiwa kwenye majukumu
ya kibunge unakuwa na hofu ya watu kwenda kufanya kampeni za kuomba kura
chinichini, mambo haya yanatunyima amani, tunashindwa kusimamia hoja. akili
yote inawaza jimboni kwako nani kaenda kuvuruga wananchi wako.
Kwa sasa wapo watu
ambao wanapita kuomba kura, huu sio utaratibu mzuri , inafanya sasa mbunge
ashindwe kukaa bungeni badala yake anaenda kupambana na watu wanaopita kwenye
majimbo bila hata kampeni kuanza, naomba chama kiangalie majimbo ambayo
yanavamiwa na watu.
Raia Tanzania: Kupitia mahojiano haya, unakipi cha kuwaeleza
wananchi wako?
Dk.Kikwembe: Kikubwa niwaombe wananchi wangu, wapiga kura
wangu wa Jimbo la Kavuu kuwa wajaribu kutambua sheria zilizopo kwenye
halmashauri ili tuweze kusonga mbele.
Lakini pia
niwahakikishie umeme unakuja muda sio mrefu, Rais Dk. Magufuli amekuwa akisisitiza
kuwepo kwa umeme vijijini na mimi mbunge wao nipo katika kulisimamia hilo,
kikubwa wajiandae na kuwa na matumizi mazuri hususan kulinda miundombinu.
Kama mbunge wao nipo katika harakati za kuhakikisha
changamoto sugu zilizopo katika jimbo ninazifanyia kazi.
JIUNGE
NASI , BONYEZA
HAPA http://www.raiatanzania.blogspot.com ku-install App ya
raiatanzania, bila
ya kuingia website Tweet@Raia
Tanzania online, youtube@Raia Tanzania online TV, Fb@Raia Tanzania online,
insta@raia Tanzania online