`Maji ya chooni ni dili’
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/maji-ya-chooni-ni-dili.html
JAMII imeshauriwa kujiunga kwenye vikundi ili kuunganishwa kwenye mfumo wa teknolojia ya usafishaji wa maji taka kwa ajili ya matumizi mengine ili mfumo huo uwasaidie kutumia maji hayo kwa shughuli mbalimbali zenye tija badala ya kuyateketeza baada ya matumizi.
Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa ufundi wa kampuni ya kuhamasisha matumizi endelevu ya maji taka (OSWAMS), Juma Mohamed Nasoro katika ziara ya maofisa mbalimbali wa serikali walipokuwa wakitembelea mradi huo unaotekelezwa katika nyumba za maofisa wa jeshi la polisi, mikocheni jijini Dar es Salaam.
Alisema tekonolojia ya usafishaji wa maji taka ni muhimu wakati huu taifa likihitaji watu wake kuwajibika ipasavyo kwa kuanzisha miradi ya uzalishaji mali kufikia uchumi wa kati kwa njia ya viwanda.
Kwa bahati mbaya, sehemu kubwa ya watu hawajatambua fursa zilizopo katika matumizi ya teknolojia hiyo na kusababisha maji taka yanayozalishwa kuteketezwa wakati yangetumika kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji wa samaki, ujenzi na bustani.
“Maji machafu ni fursa sio tatizo. Kwa hali ilivyo sasa kila hitaji la maji lazima yatumike maji ya Dawasco. Tunataka maji taka yasafishwe na yatumike kwa shughuli za kuongeza kipato sio kutegemea maji ya Ruvu chini na Juu. Ili kufikia malengo haya ni lazima elimu ipelekwe kwa wananchi ya umuhimu wa teknolojia hizi ambayo pia huzuia magonjwa hasa ya mlipuko,”alisema.
Akifafanua kuhusu mfumo huo wa kutibu maji taka, Nasoro alisema kabla ya maji hayo kutumika hupitia hatua kadhaa kuanzia utengenezaji wa chemba ambayo ni ya kwanza ya matibabu ya maji hayo.
Kisha maji taka hupitishwa kwenye mfumo wa pili wa tiba unaojulikana kitaalamu kama anaerobic (ABR) na U-Flow Anaerobic (UAF ) ambapo wadudu hula takataka kabla ya kufikia kiwango cha juu cha udhibiti, alisema.
“Maji yanayotibiwa kwa njia hizo yanakuwa yametibika kwa asilimia 85 na kiasi kingine huenda aridhini. Kwa hali hii sio rahisi kusababisha magonjwa, ni salama kwa matumizi kwani yamesafishwa kitaalamu. Yanafaa sana kwa kilimo na ufugaji kwani yana mbolea, nitrogen na phosphorus,”alisema.
Alisema kampuni yake imefanikisha teknolojia hiyo katika taasisi za umma na shule binafsi ya Libermann ya pia ya jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya maofisa waliotembelea mradi huo kutoka wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Jiji la Dar es Salaam na Manispaa za Kinondoni, Ilala, Temeke na Ubungo waliridhishwa na utekelezwaji wa mpango huo na kusema hatua inayotakiwa ni jamii kuhamasishwa kujiunga baada ya kuutathimini na kuingizwa kwenye mipango ya ya serikali.
Afisa afya wa Manispaa ya Ubungo Wilson Msangi alisema teknolojia hiyo ni hupunguza gharama ya ukusanyaji wa maji taka, huchukua nafasi ndogo na kushauri Halmashauri kuihamasisha kwenye maeneo kama shule na hospitali kutokana na maeneo hayo kuzalisha kiasi kingi cha maji taka.
JIUNGE
NASI , BONYEZA
HAPA http://www.raiatanzania.blogspot.com ku-install App ya
raiatanzania, bila
ya kuingia website Tweet@Raia
Tanzania online, youtube@Raia Tanzania online TV, Fb@Raia Tanzania online,
insta@raia Tanzania online