Maalim Seif mwanasiasa nguli anayecheza na akili za wafuasi wake

Na Umar Mukhtar, Zanzibar,


HAKUNA mwanasiasa mwenye uwezo na maarifa ya kucheza na akili, mawazo au  fahamu za wanachama na wafuasi wake Barani  Afrika  anayempita Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad .
 
Maaalim Seif
Hakuna na hatokei mwanasiasa wa aina hiyo Tanzania, Afrika Mashariki na Kati na pengine katika Bara zima la Afrika au duniani kote mwenye uwezo wa aina hiyo, labda yule mtumishi wa kiroho Kibwetere wa Uganda .

Mwanasiasa huyo ana uwezo mkubwa sana  tena  wa ajabu wa kuwaambia wanachama wake huku akiwaonyesha rangi nyueusi na wakati huohuo akiwataka waamini na kukubali ni manjano nao wakafuata kama dagaa wanaomulikiwa na mwanga wa karabai. 

Ana jeuri ya kuwaeleza acheni mara moja msishiriki uchaguzi nao wakajitoa. Amewahi kusema  rais mstaafu wa Zanzibar, Dk. Salmin Amour  Juma, ataondoka madarakani kabla ya mwaka 2000 nao  wakakubali huku wakipita mitaani na kusema mwezi ujao, kesho, kesho kutwa na mtondogoo Dk. Salmin ataondoka .

Amewahi kudai amekamata mkanda wa maneno unaelezea mpango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) chini  ya Rais mstaafu Dk. Salmin Amour kuna njama ya kutaka kumuua .Mwandishi galacha wa habari Ali Saleh Alberto akaandika na kutangaza moja kwa moja kupitia ya BBC .

Maaalim Seif aklipotakiwa kuonyesha mkanda huo kama ushahidi, akarukaa kimanga  na kusema atauonyesha akifikishwa Mahakamani.
BBC London wakalazimika kumlipa mamilioni ya fedha Dk. Salmin nje ya mahakama.
Amewahi kuwaambia wanachama wa Cuf na wananchi wa Zanzibar ikiwa atachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar ataleta mabadiliko ya kiuchumi ndani ya siku 100, lakin I alipoteuliwa kushima Umakamu wa Kwanza wa Rais na mshauri namba moja wa Rais, ameshindwa kumsaidia Rais Dk. Ali Mohamed Shein kuleta neema hiyo.

Amewahi kuwazuia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa chama chake wasichangie hoja yoyote ndani ya Baraza la Wawakilishi wakati wa tawala za Dk. Salmin na Dk. Amani Karume, nao wakakubali huku wenzao CCM wakipitisha miswaada mbalimbali na kuwa sheria. 

Ameshawahi kusema Dk. Amani Karume atang'oka madarakani kabla ya mwaka 2010 kwasababu ameiba kura zake. Wafuasi wake wakaamini. Mwishowe Dk. Karume akamwachia kijiti Dk. Ali  Shein na yeye hadi leo hajaulizwa lolote na wafuasi hao.

Uhodari na maarifa ya Maalim Seif ni ya kipekee kabisa .Huenda yanampita hata yule mwanamke aliyejitangaza ni Mtume wa Mungu kule Uganda, Alice Akwema na kuwaeleza wafuasi wake wa kiroho atakayekunywa maji ya utukufu wake hatakufa kwa kupigwa risasi 

Hebu tazama ili ujionee.Tokea ufanyike uchaguzi wa Zanzibar wa mwaka 2015 na kurudiwa tena Machi, 2016, amekuwa akiwaaminisha wanachama wake kuwa Dk. Shein ataondolewa madarakani nay eye ndiye atakayekuwa Rais mpya wa Zanzibar.

Mashabiki na wanachama wake wanakubali na wengine wakipiga vigelegele.
Huko Pemba wala usiseme. Wake kwa waume wanajenga majukwaa ya sherehe wakisubiri ushindi wa Maalim Seif ambao namna ya kushinda kwake na kuwa Rais hakufikiriki wala kusadikika .

Ukitaka kumjua Maalim Seif ni mwanasiasa kiboko yao,  tazama alivyowahi kumshambulia Rais mmoja mstaafu wa Zanzibar, mkewe, wanawe na  shemeji yake lakini cha kustajaabisha watu hao walionangwa leo ndiyo washirika wake wa karibu. 
Maalim Seif amewahi kusema  Zanzibar kuna ufisadi unaofanywa na ‘The first family’ ukiongozwa na Rais huyo mstaafu. Akasema anapora fukwe, mashamba, nyumba za umma na viwanja, wanawe akiwamo binti yake wanapata zabuni SMZ kinyume cha taratibu za kisheria, huku wakijipatia mamilioni ya fedha. 

Hakuishia hapo, akaeleza kuwa shemeji yake mmoja Rais huyo mstaafu amejenga majumba ya kifahari katika kijiji cha familia  yake kutokana na kuiibia serikali.
Kinachowashangaza watu watu hao wote sasa ndio wapiga debe  wa mwanasiasa huyo.
Ameshawaeleza hata wasomi wenye maarifa na elimu ua juu akiwamo, Juma Duni Haji, aliyemtaka ahamie Chadema ili awe mgombea mwenza wa, Edward Lowassa. Duni baada ya kupoteza sifa ya uanachama ndani ya Cuf akashindwa kuwania umakamu mwenyekiti wa chama hicho. 

Maaslim Seif alivyo na jeuri ya kisiasa akasimamia sakata mwenyekiti mwanzilishi wa chama hicho, James Mapalala, akafukuzwa uanachama, akawatimua kwa nyakati tofauti viongozi waandamizi na waasisi wa Cuf akiwamo  Naila Majid Jidawi, Juma Othman Juma na Salum Msabah Mabarouk, Shaibu Akwilombe na Tambwe Hiza wala hakuna aliyepinga na kusema hivyo sivyo.
Maalim kwa misuli ya kisiasa aliyonayo amethubutu kumtosa aliyekuwa msemaji hodari na mahiri wa Cuf, Ramadhan Mohamed Mzee, mwanasiasa muasisi aliyetumia fedha na wakati wake, Hamad Rashid Mohamed, akafuata aliyekuwa kiongozi wa upinzani bungeni Fatma Maghmbi na kumalizia kumtosa muasisi wa Kamahuru, Mussa Haji Kombo .

Huyo ndiye Maalim Seif Sharif Hamad, aliyewahi kuwa katibu maalum wa  Rais wa Zanzibar, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, aliyemteua akawa Waziri wa Elimu  wa SMZ hadi kufikia  Waziri Kiongozi baadae CCM ikashindwa kuvumilia  na kumfukuza uanachama  mwaka 1987. 

Huyo ndiye Maali Seif  anayezichezea akili za wanachama wake huku akiwaambia mwishoni mwa Septemba hii Dk. Shein anaondolewa madarakani.
NijuavyO, Rais Dk. Shein ataabaki katika kiti chake  na MaaliM seif ataibuka  na CD  nyingine mpya itakayochezwa na wanachama wake hata kama santuri hiyo itakuwa ni zilipendwa. 


JIUNGE NASI , BONYEZA HAPA http://www.raiatanzania.blogspot.com ku-install App ya raiatanzania,  bila ya kuingia website Tweet@Raia Tanzania online, youtube@Raia Tanzania online TV, Fb@Raia Tanzania online, insta@raia Tanzania online

Related

SIASA 5449599858941640695

Post a Comment

emo-but-icon

item