Mufti Tanzania, Zanzibar kupamba Kongamano la Misk ya Roho
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/mufti-tanzania-zanzibar-kupamba.html
MUFTI wa Tanzania Sheikh Abubakar Zubeir pamoja na
Mufti wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kaabi, ni miongoni mwa wageni mashuhuri
watakaohudhuria kwenye kongamano kubwa la Kida’awa
la Afrika Mashariki lijulikanalo kama ‘Misk ya Roho.
Kongamano
hilo ambalo ni la kwanza na la aina yake, limepangwa kufanyika Jumapili ya Novemba
26 mwaka huu katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Taj Mohammed
Abbas, Mkurugenzi wa makongamano wa Taasisi ya
The Islamic Foundation (TIF), ambayo ndiyo inaandaa kongamano hilo amesema,
pamoja na mambo mengine, Mufti Zubeir na Mufti Kaabi watawasilisha mada kwenye
kongamano hilo.
Mufti, Sheikh Zubeir
Sheikh
Abubakar Zubeir ni Mufti wa tatu na alichaguliwa mwaka 2015 baada ya kifo cha
mtangulizi wake Sheikh Shaaban Simba, ambaye alipokea kijiti cha wadhifa huo
kutoka kwa Muftiwa kwanza wa Tanzania, Sheikh Hemed bin Jumaa bin Hemed.
Mufti
Zuberi ni mzaliwa wa Tanga na kwa muda wa miaka 22 iliyopita, kabla ya kuwa
Mufti, amekuwa kiongozi na kushikilia nyadhifa mbalimbali ikiwamo pamoja na
Naibu Mufti wa Tanzania na Mjumbe wa Baraza la Ulamaa.
Nafasi
nyingine ambazo Sheikh Zubeir aliwahi kuzihudumu ni pamoja na Msaidizi wa Mufti
wa kwanza wa Tanzania, Sheikh Hemed bin Jumaa bin Hemed kuanzia mwaka 1984 hadi
2002, Naibu Kadhi Mkuu wa Tanzania, na Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya BAKWATA.
Mufti, Sheikh Kaabi
Sheikh
Saleh Omar Kaabi aliteuliwa kuwa Mufti wa Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Dkt.
Ali Mohammed Shein tangu mwaka 2011 baada ya kifo cha mtangulizi wake Sheikh
Harith bin Khelef.
Mbali
na kuwa Mufti, kwa sasa Sheikh Kaabi ni kiongozi katika Baraza la Maulamaa wa Zanzibar,
ambalo kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar lina uwezo wa kutoa maamuzi juu ya
masuala mbalimbali ya dini ya Kiislamu visiwani humo.
Sheikh AbdulQadir
al-Ahdal
Mbali
na viongozi hao wakuu wa dini ya Kiislamu hapa nchini, pia kongamano hilo
litahudhuriwa na Rais wa taasisi ya Al-hikma Foundation, Sheikh AbdulQadir bin Muhammad
Ahmad al-Ahdal ambayo inamiliki shule kadhaa za ngazi za awali, msingi na
sekondari.
Sheikh
AbdulQadir ambaye kwa sasa ni raia wa Tanzania, kabla ya kuja nchini, mnamo
mwaka 1992 alianzisha Madrasa za kusoma na kuhifadhi Qur’ an katika Mkoa wa
Hadharamout nchini Yemen chini ya usimamizi wa mwalimu wake Sheikh Ahmad Hassan
al-Mualim.
Pia,
Sheikh AbdulQadir ni Mwanazuoni anayejishughulisha na tafiti za Kifiqh, na
wakati huo huo ni Mjumbe wa Kamati ya Fatwa katika Umoja wa Wanazuoni wa
Kiislamu hapa nchini (Hay-at).
Kando
na hayo, Taasisi ya Alhikma Foundation ambayo Sheikh AbdulQadir ndiye Rais
wake, imekuwa ikiandaa na kusimamia mashindano makubwa ya kusoma na kuhifadhi
Qur’an hapa nchini kwa kushirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati.
Aidha,taasisi
anayoiongoza ya Alhikma Foundation hutoa huduma za kijamii kama vile kuchimba
visima nk.
Mtoto aliyemlingania
Kenyatta
Mgeni
mwingine ambaye anatarajiwa kuvuta hisia za Waislamu wengi katika kongamano
hilo, ni mtotoOmar Mohammed kutoka nchini
Kenya.
Omar
ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 6, aliwahi
kukutana na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta katika Ikulu ya Mombasa ambapo alitumia
fursa hiyo kumlingania ili awe Muislamu.
Baadhi ya wasomi na wachambuzi wa masuala ya dini ya Kiislamu
hapa nchini wanamuelezea Omar kama mtoto jasiri, mwerevu na mwenye fikra pana
kutokana na uthubutu wake wa kumshawishi kiongozi wa ngazi ya juu katika nchi
kujiunga na Uislamu.
Masheikh
wengine watakaohudhuria kwenye kongamano hilo ni Sheikh Salim Barahiyan kutoka
Tanzania, Sheikh Juma Amir kutoka nchini Kenya,Sheikh Ibrahim Kyebanja kutoka
Uganda na Sheikh Zuberi Bizimana kutoka Rwanda.
Wengine
ni Sheikh Jamal Maboyi (Burundi), Sheikh Muhammad Issa (Tanzania), Sheikh Yusuf
Abdi (Kenya) na Sheikh Nurdin Kishki kutoka Tanzania.
Katika
hatua nyingine, Mkurugenzi wa Makongamano ya TIF, TajMohammed Abbas aliwashajiisha
Waislamu kuhudhuria kwa wingi kwenye kongamano hilo ili kujifunza mambo muhimu
ya dini yao ikiwa ni pamoja na umuhimu wa kutunza amani.
Mada zitakazowasilishwa
“Mada
kama vile Ikhlas, umuhimu wa elimu na thamani ya amani japo sio maudhui mpya
kuzungumzwa au hata kuandikwa, lakini zina umuhimu mkubwa hususan kwa Waislamu
wa zama hizi. Tunaamini kupitia kongamano hili Masheikh watazidadavua kwa namna
yao na kwa misingi inayokubalika kwa faida ya Waislamu na jamii kwa ujumla,”
alisema TajMohammed.
TajMohammed
alifafanua kuwa, amani, utulivu na umoja ni mambo yanayojenga mustakabali na
hadhi ya mwanadamu kuanzia katika maisha binafsi na mbele ya jamii nyingine,
hivyo lazima amani itunzwe na ienziwe ili idumu katika uasili wake.
TajMohammed
aliongeza:“Kuwepo jamii ya mwanadamu ni jambo la msingi na la umuhimu mno, kwa
kuwa binadamu ni mwanajamii katika maumbile yake, anazaliwa katika jamii,
anaishi na kufia humo,”.
Tiketi
Aidha
TajMohammed aliwakumbusha Waislamu kuendelea kujisajili kwa ajili ya kongamano
hilo kwa kununua tiketi kwa shilingi 5,000 kupitia namba 0787 565777, 0773
565777, 0718 000433 na 0742 877775 na kwamba kiasi hicho kitajumuisha huduma ya
chakula pamoja na vinywaji.
Alivitaja
vituo vya kununulia tiketi hizo kuwa ni pamoja na Discount Center- iliyopo
Mlimani City na katika mtaa wa Uhuru, Gem Point iliyopo mtaa wa Indira Gandhi,
Baby Shop iliyopo GSM Mall Msasani, Kanzu Point iliyopo City Mall na Taste Me
iliyopo Dar Free Market.
Sehemu
nyingine ni GGS Bolts & Nuts iliyopo mtaa wa Livinstone Kariakoo, Her
Finess iliyopo Barabara ya Umoja wa Mataifa, Dayun Shop iliyopo Puma Fuel
Station Tabata, Babyz World Tanzania iliyopo mkabala na kituo cha polisi
Msimbazi na Peace Travel iliyopo Mtaa wa Manyema Kariakoo.