Kalaghe:Mchuuzi wa makasha hadi Mkurugenzi
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/kalaghemchuuzi-wa-makasha-hadi.html
KILA mtu ana historia yake katika maisha, yawe hasi au chanya. Na hapo ndipo hutimia neno la kitaalamu lisemalo: `life is a process’ au maisha ni mchakato, hatua.
Laibai Kallaghe haisau hatua za maisha yake kutoka wazo la biashara ya kutengeneza na kuuza mabegi ya shule aliyoyatengeneza kienyeji kwa kutumia vipande vya makasha (maboksi) zaidi ya miaka 50 iliyopita huko Korogwe mkoani Tanga hadi kuwa Mkurugenzi mtendaji katika miaka ya hivi karibuni.
Mkuregenzi wa SKUVI, Laibai Kalaghe (Mwenye shati jeupe kulia,) akiteta jambo na muasisi wa vikundi vya SKUVI Mwenyekiti mtendaji wa IPP Dk. Regnard Mengi (kushoto). |
Kwake yeye, biashara huanza na wazo kisha kulichakata kwa kutumia juhudi zako binafsi kwasababu unalipenda wazo hilo na lazima uishi kwalo ili kufikia malengo ya wazo hilo.
Kwa msingi huyo, anasema yeye si mtu mwenye kuzembea wazo lazima alifuatilie na bila kukata tama hata kama zitajitokeza tambo ambazo huweza kuangusha wazo lake.
Kallaghe alianza wazo la biashara tangu akisoma shule ya msingi huko kijijini kwake Korogwe baada ya kubaini kuwa katika shule alimokuwa akisoma kuna hitaji la mabegi kwa wanafunzi wenzake.
Hiyo ikamsukuma kutafuta maboksi ya karatasi ngumu, kuyaunda na kupata mabegi ambayo alianza kuwauzia wanafunzi wenzake shuleni hapo na shule za jirani baada ya kuvutiwa na mabegi hayo.
Baadaye aliogundua kwamba mabegi hayo ya makasha yanahitaji kuongezewa kitu fulani, kuyafanya yapendeze zaidi na kuongezeka thamani. Yeye aligundua kwamba ili mabegi hayo yapendeze, kupendwa zaidi na kuongezeka ayapambe kwa nje kwa kuzungusha vipande vya magazeti ya kichina aliyopatiwa na marafiki zake waliokuwa Jijini Dar es Salaam.
Ubunifu wake huo ulimsaidia kuongeza kipato na kufanikiwa kupata mtaji wa kuanzisha biashara nyingine ya kuuza bidhaa ndogondogo kama vile mbogamboga, aliyoendelea nayo hadi ilipoanza elimu ya sekondari katika kituo cha elimu ya watu wazima, Korogwe.
Yungali yupo sekondari, anasema aliendelea na biashara yake hiyo na kufanikiwa kugawa mtaji kwa kuanzisha biashara ya kuuza peremende kutoka Kenya zilizojulika kama BigG na sigara kwa njia ya uchuuzi. Aliuza sana wakati wa sherehe kwa kutembea hadi huko hasa wakati wa usiku kwenye muziki maarufu kama disko hadi mwaka 1979 alipohitimu elimu ya sekondari huku akiendelea na biashara zake.
Kallage alihamia jijini Dar es Salaam mwaka 1984 na kujiunga na chuo cha ufundi Dar es Salaam (DIT) kwa kozi ya kuu ya uhandisi (General Course Engeneering) katika fani ya uchoraji.
Baada ya kuhitimu mafunzo hayo, alijiunga na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) katika chuo cha Tanzania Motor Service kilichopo cha mkoani Arusha na kupata cheti cha Motor Cycle technical daraja la kwanza na baadae elimu mbalimbali ya ujasiriamali.
“Pia nilifanikiwa kusoma stashahada ya elimu ya usimamizi wa biashara kwa ujasiriamali wangu niliweza kusoma na kufanya kazizangu, saa kumi na moja jioni nafunga kazi na kuelekea darasani hadi saa tatu usiku…wengi waliniona kama anacheza kwa kuwa mtu anawezaje kusoma huku anajishughulisha na ujasiriamali,”alisema.
Mwaka 1995 alianza ufundi wa magari mtaani. Alikuwa hana uhakika wa kupata kazi, jambo lililomsukuma kubuni njia ya kupata kazi.
Anasema aliamua kupanga makopo matupu ya oili pembeni mwa barabara ya zamani ya Bagamoyo ili kuwavuta watu, hasa walioharibikiwa na magari. “Ndipo siku moja, raia mmoja wa kigeni, akaona yake makopo na kushuka kutoka ndani ya gari.
Kisha nilimsogelea na kugundua kuwa gari yake ilikuwa na hitilafu ilisababisha isiwake, niliitengeza na kulipwa pesa, ambayo kwangu ilianza kuwa mtaji,”alisema.
“Baadae Dk. Reginald Mengi alitangaza kukutana na vijana kwa hiari kwa kauli mbiu yake aliyoiita `NIFANYE NINI?’ ambayo ni fursa. Alifanya nao mkutano kwa dhamira ya kuwasaidia vijana ili waweze kujiajiri wenyewe na kutoa fedha kwa vikundi 550 vya Shujaa wa Kupiga Vita Umasikini (SKUVI) yeye akiwa kikundi namba 141 na kila kikundi kilipatiwa Sh.25,000.
Anasema aliamua kwenda Kariakoo kununua mashine ya kuchaji betri za magari na kwa kujiunga na mwenzake mmoja ili tufanye biashara pamoja.
“Wakati huo umeme ulikuwa bado haujasambaa maeneo mengi hivyo nilikuwa nauza oil na kuchaji betri ya magari, baada ya faida na nikaenda kununua mashine za uchomeleaji” Kwa mtaji huo walifanikiwa kuanzisha kituo cha kutengeneza magari (gereji), kununua mitungi ya gesi na kupaka rangi magari na kupokea oda kwa watu mbali mbali.
Wakabuni utengenezaji wa matoroli kwa ajili ya kusambazia maji na wanaofanya usafiKutokana na kukua kwa biashara hiyo baadhi ya benki kama Baclays na Akiba walimuamini na kumkopesa mtaji ambao ulimuwezesha kuteneneza matokoli hayo ya aliyoyapeleka kwenye maonesha ya biashara sabasaba, na kufanikiwa kukuza mtaji.
Kallaghe ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Skuvi 141 inayotamba kwa jina la Mr. Oil anasema alianza kujenga mahusiano ya kibiashara kwa kushirikia maonyesho ya biashara nchini China ambako alijifunza mbinu mbalimbali ya biashara yake ya uchomeleaji wa kisasa.
Ziara hizo zilimpa nafasi ya kujuana na watu mbalimbali ambao hadi sasa anashirikiana nao, yeye akiwa sehemu ya wakala wa kuuza bidhaa kutoka nchini humo, huku yeye akiagiza na kuuza katika soko la ndani.
Katika taasisi yake ya SKUVI ameweza kuwafundisha vijana zaidi ya 20 kwa kazi hiyo ya uchomeleaji ambao wengi wao kwasasa wanajitegemea na kuwa tegemeo
kwa familia zao. Pia ni mwalimu wa ujasiriamali.
Juhudi hizo zimemfanya kuendesha maisha yake, kumiliki gari, nyumba, kusomesha watoto hadi elimu ya chuo kikuu. Pia Kujenga mahusiano makubwa na kampuni za ndani na watu mbalimbali. Anashauri vijana na watu wengine, kuwa wabunifu, kutumia mawazo yao vizuri na kufanya kazi bila kukata tamaa Soma Zaidihttps://lenzimedia.blogspot.com/search/label/GURUDUMU%20LA%20MAISHA