JAPAN YAONESHA NIA KUI JENGA DODOMA KWA MIUNDOMBINU YA KISASA
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/japan-yaonesha-nia-kuijenga-dodoma-kwa.html
SHIRIKA la Kimataifa la Maendeleo la Japan (JICA) limesema liko tayari kushirikiana na Serikali kujenga miundombinu ya kisasa ya usafiri, Nishati ya umeme, maji na usafi wa mazingira katika Makao Makuu ya nchi, Dodoma.
Ahadi hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Shirika hilo Bw. Hiroshi Kato wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, Jijini Dar es Salaam.
Bw. Kato alisema kuwa mradi mwingine wanaotaka kuutekeleza katika mji wa Dodoma ni udhibiti wa taka ngumu na kwamba wanachosubiri ni Serikali kuainisha maeneo ya vipaumbele vilivyoko katika mpango mji wa Dodoma.
Aidha Makamu huyo wa Rais wa JICA alisema kuwa Shirika lake litaendelea kusaidia eneo la kilimo hususan kilimo cha mpunga ili kuongeza thamani ya zao hilo na kuwakomboa wakulima.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango amelishukuru Shirika hilo kwa kuonesha nia ya kusaidia ujenzi wa mji wa Dodoma ambao ndio Makao Makuu ya nchi.
Alisema kuwa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa kuupanga mji wa Dodoma mapema ili kuondoa changamoto za msongamano wa huduma za jamii kwenye eneo moja kama ilivyo Jijini Dar es Salaam.
“Pamoja na umuhimu wa miundombinu ya maji, umeme, usafiri wa mjini, lakini pia tunataka tujenge mapema njia za juu (ring roads) ili kudhibiti msongamano wa magari” alisema Dkt. Mpango.
Aliongeza kuwa mradi mwingine wa kipaumbele katika mji huo ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa katika eneo la Msalato, karibu kilometa 20 kutoka katikati ya mji huo ili kurahisisha usafiri kwa njia ya anga.