CCM, Chadema kuchuana uchaguzi wa ubunge Januari.
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/12/ccm-chadema-kuchuana-uchaguzi-wa-ubunge.html
WAKATI vumbi
la kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mdogo wa Madiwani katika kata 43 za mikoa 19 ya
Tanzania Bara, likiwa halijatulia, vumbi jingine la uchaguzi mdogo linatarajiwa
kutimka mapema mwezi ujao katika majimbo matatu ya ubunge na kata sita.
Novemba 26, mwaka huu, kulifanyika Uchaguzi
Mdogo wa Madiwani katika kata 43 za mikoa 19 ya Tanzania Bara, ambao
ulishuhudia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikizoa kata 42 kati ya hizo na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika uchaguzi uliokuwa na mtifuano mkubwa.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) jana
ilitangaza kuwa Januari 13, mwakani kutafanyika Uchaguzi Mdogo katika majimbo
ya Longido katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido mkoani Arusha, Songea Mjini
katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma na Singida Kaskazini
katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida mkoani Singida.
NEC imezitaja kata ambazo ziko wazi kuwa ni
Kimandolu (Halmashauri ya Jiji la Arusha), Kihesa (Halmashauri ya Manispaa ya
Iringa), Bukumbi (Halmashauri ya Wilaya ya Uyui), Kurui (Halmashauri ya Wilaya
ya Kisarawe), Keza (Halmashauri ya Wilaya ya Ngara) na Kwagunda (Halmashauri ya
Wilaya ya Korogwe).
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari
jana, Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mkuu mstaafu Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid
alisema walipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge kuhusu kuwapo kwa nafasi wazi
za majimbo ya uchaguzi ya Singida Kaskazini Mkoa wa Singida kuanzia Oktoba 30,
mwaka huu.
Alieleza kuwa hiyo ilitokana na aliyekuwa
Mbunge wa jimbo hilo, Lazaro Nyalandu, kuvuliwa uanachama na CCM, hivyo kwa
mujibu wa Ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya
mwaka 1977, alipoteza sifa ya kuwa mbunge.
Ibara hiyo inaeleza kuwa “Mbunge atakoma
kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge – iwapo Mbunge ataacha kuwa mwanachama
wa chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa Mbunge”.
Alisema kuwa Jimbo la Uchaguzi la Songea
Mjini mkoani Ruvuma, liko wazi kuanzia tarehe 24 Novemba, 2017 kufuatia kifo
cha aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo, Ndugu Leonidas Tutubert Gama.
“Aidha, kwa mujibu wa kifungu cha 113(1)(2)
cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura ya 343, Tume imepokea Hati kutoka Mahakama
Kuu Kanda ya Arusha, ikithibitisha kuwa Jimbo la Longido Mkoa wa Arusha lipo
wazi kuanzia tarehe 30 Oktoba 2017 kufuatia Mahakama Kuu kufuta matokeo ya
uchaguzi wa jimbo hilo na hivyo Ndugu Onesmo Ole Nangole aliyekuwa Mbunge wa
Jimbo hilo kupoteza sifa za kuwa Mbunge,” alieleza Jaji Mkuu mstaafu Hamid.
Akielezea taratibu za mchakato huo wa
uchaguzi, Makamu Mwenyekiti wa NEC alisema fomu za uteuzi katika majimbo ya
Singida Kaskazini na Longido na kata za Keza, Kimandolu, Kwagunda, Bukumbi,
Kurui na Kihesa, zitatolewa kati ya Desemba 12 hadi 18, mwaka huu.
Kwa Jimbo la Songea Mjini, fomu za uteuzi
itakuwa kati ya Desemba 14 hadi Desemba 20, mwaka huu. Kuhusu uteuzi, alisema
wagombea katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido na kata za Keza,
Kimandolu, Kwagunda, Bukumbi, Kurui na Kihesa, utafanyika Desemba 18, mwaka
huu; wakati kwa Jimbo la Songea Mjini itakuwa Desemba 20, mwaka huu.
Aidha, taarifa hiyo ya NEC ilieleza kuwa
kampeni za Uchaguzi Mdogo katika majimbo ya Singida Kaskazini na Longido na
kata za Keza, Kimandolu, Kwagunda, Bukumbi, Kurui na Kihesa zitaanza Desemba
19, mwaka huu na kumalizika Januari 12, 2018.
Ilieleza kuwa kampeni za Uchaguzi Mdogo
katika Jimbo la Songea Mjini, zitaanza Desemba 21, mwaka huu na kumalizika
Januari 12, 2018, siku moja kabla ya uchaguzi katika majimbo hayo matatu na
kata sita.
“Tunavikumbusha vyama vya siasa na wadau
wote wa uchaguzi wazingatie Sheria, Kanuni, Taratibu, Miongozo na maelekezo
yote wakati wa kipindi cha Uchaguzi Mdogo wa majimbo matatu na kata sita,”
ilieleza NEC.
Kata 43 zilizofanya uchaguzi wa madiwani
hivi karibuni na majina ya mikoa kwenye mabano ni: Murieti, Moita, Musa,
Ambureni, Ngabobo, Maroroni, Leguruki na Makiba (Arusha), Mbweni, Kijichi na
Saranga (Dar es Salaam), Chipogolo (Dodoma), Bukwimba na Senga (Geita), Kitwiru
na Kimala (Iringa), Bomambuzi, Mnadani, Machame Magharibi na Weruweru
(Kilimanjaro), Chikonji na Mnacho (Lindi), Nangwa (Manyara), Ibighi(Mbeya),
Kiroka na Sofi (Morogoro), Milongodi, Reli na Chanikanguo (Mtwara), Kijima na
Mhandu (Mwanza), Sumbawanga (Rukwa), Lukumbule, Kalulu na Muongozi (Ruvuma),
Siuyu (Singida), Nyabubinza(Simiyu), Ndalambo (Songwe), Nata na Muungano
(Tabora) na Majengo, Lukuza na Mamba (Tanga). Mbali na CCM na Chadema, vyama
vingine vinavyotarajiwa kusimamisha wagombea ubunge na udiwani ni pamoja na
Chama cha Wananchi (CUF), NCCRMageuzi, ACT-Wazalendo, UDP na UPDP.