Meya Mwita asaini mkataba kurudisha uhusiano mpya na jiji la Hamburg
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/meya-mwita-asaini-mkataba-kurudisha.html
MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amefungua ukurasa mpya wa uhusiano wa miji dada kwa kusaini mkataba mpya kati ya jiji la Hamburg na Dar es Salaam.
Mkataba huo umesainiwa Novemba 14, mwaka huu katika Jiji la Hamburg ambapo Meya Mwita na Mstahiki Meya wa Jiji la Hamburg, Olaf Scholz, walisaini mkataba huo na kushuhudiwa na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana.
Wengine walioshuhudia tukio hilo ni , watendaji wakuu wa mamlaka ya Jiji la Hamburg na Taasisi mbalimbali za Serikali katika Jiji hilo, wawakilishi wa asasi za kiraia na baadhi ya Watanzania wanaoishi jijini Hamburg.
Mkataba wa awali wa uhusiano huo ulitiwa saini mwaka 2010 na Adam Kimbisa na Ole Van Beust waliokuwa mameya wa majiji hayo katika kipindi hicho.
Mstahiki Meya na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam waliwasili katika Jiji la Hamburg kwa ziara ya kikazi na kusaini mkataba huo wakitokea katika mji wa Bonn ambako walishiriki katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi ulioandaliwa na taasisi ya Engagement Global ya Ujerumani kwa miji washirika wa Ujerumani.
Viongozi hao wawili wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam wakiwa mjini Bonn walishiriki pia katika mkutano wa mameya na magavana ambao ulikuwa sehemu ya mkutano ulioandaliwa na Umoja wa Mataifa wa COP 23 ambao umefanyika sambamba na mkutano ulioandaliwa na Engagement Global.
Kabla ya kusainiwa kwa mkataba huo, vikao vya wataalam mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Engagement Global, miji wa shirika na wataalam wa Wizara ya Maendeleo ya Miji na Makazi wa Jiji la Hamburg, vilifanyika mjini Bonn na Hamburg kwa usimamizi wa Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam na Mtendaji Mkuu wa Jiji la Hamburg, Wolfgang Schmidtz,.
Aidha katika mkutano huo walibaini maeneo mengi zaidi ya ushirikiano kati ya miji hiyo, wahusika na miradi mipya inayoweza kutekelezwa kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi kupitia uhusiano huo.
Pande hizo mbili, hasa kwa kuzingatia matwaka ya Dar es Salaam, zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya mabadiliko ya tabia nchi ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo, upangaji wa miji, uboreshaji wa huduma za usafiri wa umma na shughuli za kukuza utalii katika Jiji la Dar es Salaam.
Hata hivyo baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, viongozi hao wa Jiji la Dar es Salaam walikutana na Bodi ya Ushauri ya Jiji la Hamburg na kisha kuwa na mkutano mwingine na wadau wa uhusiano huo wakiwemo Watanzania wanaoishi Hamburg ambao wajumbe wote kwa ujumla walisisitiza kila upande ufanye jitihada za dhati za kuimarisha ushirikiano huo kwa kuacha urasimu.
Hii ni safari ya kwanza ya kikazi nje ya nchi kwa Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Mwita na Mkurugenzi wa Jiji hilo, Sipora Liana, kusafiri pamoja na kurejea nchini wakiwa wamefanikiwa katika kutimiza malengo ya safari yao mjini Bonn na Hamburg