Watumishi elfu 37 kunufaika na mpango huu wa viwanja ulioanzishwa na RC Makonda
http://raiatanzania.blogspot.com/2017/09/watumishi-elfu-37-kunufaika-na-mpango.html
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda ametangaza mpango kabambe wa kuwasaidia watumishi wa umma kutokana na kazi ngumu wanazozifanya za kulitumikia taifa la Tanzania.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam RC Makonda ameeleza kuwa watumishi wa kada za elimu, afya na ulinzi wanafanya kazi kubwa mpaka inafikia hatua wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa makazi yao.
Hivyo RC Makonda kupitia wadau amefanikisha hilo ambapo watumishi wa umma kwenye kada tatu tajwa hapo juu wataweza kuuziwa kiwanja kwa kiasi cha shilingi 4000 kwa kipimo cha square meter moja na watapewa hati ya umiliki wa kiwanja.
" Kwa kawaida square meter moja ya kiwanja huuzwa shilingi 15000 hivyo watumishi hawa watauziwa kwa kiasi cha shilingi 4000 na watalipa kwa muda wa miaka mitano pindi watakapo ingia makubaliano" Alisema RC Makonda.
RC Makonda ameeleza kuwa mpango huo kabambe utanufaisha takribani watumishi elfu thelasini na saba (37,000) huku akieleza kuwa tayari watumishi 700 wameanza kunufaika na mpango huo.
RC Makonda amesema serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli itaendelea kuboresha maisha ya watumishi wa umma kwani wanamchango mkubwa kwa taifa.
" Mpango huu ni rahisi sana yaani kiwanja cha milioni tatu mpaka tano unaweza kulipa taratibu kwa muda wa miaka mitano" Alisisitiza RC Makonda.