DC Mjema kushirikiana na Kituo cha michezo Jakaya Kikwete waja na mpango wa kuendeleza Sekta ya michezo Shule za Manispaa ya Ilala

https://raiatanzania.blogspot.com/2018/10/dc-mjema-kushirikiana-na-kituo-cha.html

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, amesema moja ya mipango yake kwa Sasa ni kuona Wilaya inashika Namba moja kiwilaya Katika mkoa wa Dar es Saalam.
Dc Mjema ameyasema hayo Mara baada ya kukutana na uongozi wa Kituo cha uwekezaji wa mpira cha Jakaya Kikwete Youth Park Leo.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano licha ya kutoa elimu bure lakini wameweka mpango wa kuhakikisha kila Shule inakuwa na Kiwanja cha michezo.
Amesema michezo ni Afya na kufanya mwanafunzi kuimarika kimasomo.
Aidha katika mazungumzo yake na kocha wa Mpira wa Kikapu katika kituo hicho cha Jakaya Kikwete kilichopo Kidongo chekundu Kata ya Gerezani, Bahati Mgunda, DC Mjema, amesema kutokana na ukaribu uliopo baina yao ameiagiza Manispaa kupitia Ofisi ya Afisa Elimu kutoa ushirikiano wa kuunganisha Shule zote ndani ya Manispaa na Kituo hicho.
" Hii ni fursa Hawa ndugu zangu nimeona kunahaja ya kujenga uhusiano bora, Afisa elimu nakuomba kaeni chini mratibu haya mambo mtakapofikia mtanijulisha tuone tunakwendaje" Amesema DC Mjema.
Pia ameridhishwa na huduma zinaotolewa katika Kituo hicho huku akisema wakishirikiana Manispaa ya ilala ngazi ya Shule kimichezo haitakamatika ndani na nje ya Mikoa.
Hata hivyo ameupongeza Uongozi wa Jakaya Kikwete Youth Park kwa ushirikiano wao uliowafanya kuendelea kushikilia rekodi ya kushika nafasi ya Pili katika UMISETA Mara mbili mfululizo Mkoa wa Dar es Salaam.
DC Mjema amesema anataka kuona Wilaya ya Ilala inakuwa kinara kwa kuipiku Wilaya ya Kinondini inayoonekana kuimarika kimichezo na katika kuona hilo linafanikiwa yeye pamoja na Ofisi yake watakuwa Mabalozi wazuri katika Kituo hicho kwa kufanya michezo muda wa ziada.
Wakati huo huo DC Mjema amesema kama tutazalisha Wanamichezo wazuri Katika ngazi zote ikiwamo mpira wa Miguu, mpira wa Kikapu, Mpira wa Pete na michezo mingineyo tutazalisha Wanamichezo wazuri watakao tusaidia kupeperusha bendera yetu vyema Kimataifa na kutuletea sifa kede kede Manispaa na Taifa kwa ujumla.
Amesema michezo ni ajira kama zilivyo ajira nyingine, hivyo baada ya watoto hao kuhitimu masomo yao tutakuwa tumewatengenezea wigo mpana wa ajira katika kuendesha maisha yao.
Naye Mwalimu Mkuu wa Mpira wa Kikapu, Bahati Mgunda, amemshukuru DC Mjema kwa kufika katika Kituo hicho na kujionea programu mbali mbali za Michezo zinazoendeshwa kituoni hapo.
Mgunda amesema ni jambo la faraja kwao kupata ugeni mkubwa wa Manispaa hivyo watajitahidi kuona ushirikiano wao unakuwa na faida katika kuendeleza Michezo Manispaa ya Ilala na Tanzania kwa ujumla.
Amesema wapo tayari kuziunganisha Shule zote za Manispaa bila malipo yoyote.
" Huu ni ugeni mkubwa kwetu, na sisi tuna ahidi tutaendelea kushirikiana kuona Michezo ya watoto zetu Shuleni inakuwa na kupata vipaji mbali mbali vitakavyokuwa ni Taifa la kesho" Amesema Mgunda.
Hata hivyo amemuomba DC Mjema kufika Ofisini kwake kwa ajili ya kuona fursa zaidi.