Manispaa Temeke yafanya kumbukizi kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere kwa bonanza la aina yake
https://raiatanzania.blogspot.com/2018/10/manispaa-temeke-yafanya-kumbukizi.html
MANISPAA ya Halmashauri ya Temeke, Leo wamefanya bonanza la aina yake katika kumuenzi Rais wa awamu ya kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Bonanza hilo lililofanyika kwenye Uwanja wa Taifa wa Uhuru, lilijumuisha michezo mbali mbali. Miongoni Mwa michezo hiyo ni pamoja na mpira wa miguu kwa timu ya Manispaa, Kuvutana kamba , kukimbia na magunia pamoja na kukimbiza Kuku.
Akizungumza na Waandishi wa Habari Leo , mgeni rasmi ambaye ni Kaimu Katibu Mtendaji Baraza la Michezo Tanzania ( BMT), Alex Nkenyenge, ametoa shukrani kubwa kwa Uongozi mzima wa Manispaa ya Temeke kwa kuandaa bonanza hilo lenye Lengo la kumbukumbuka baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.
Amesema kuwa Mwalimu Nyerere, alikuwa mpenzi mkubwa wa michezo ya kukimbia ( Jogging), hivyo ni jambo jema lenye kutia Hamasa kwa Vijana wa Kitanzania katika kutoa vipaumbele kwenye mchezo huo.
Aidha, amesema Afya ndio mtaji, hivyo ili mtu aweze kufanya kazi kwa ufanisi lazima awe na Afya bora.
Amesema kuwa wapo baadhi ya watu wanaosemea vibaya Jogging lakini amefafanua kwamba mchezo huo sio wa kipuuzi bali ni mchezo kama ilivyo michezo mingine yenye mlengo wa kuzalisha Mali na wajasiriamali.
" Wapo baadhi yetu wanadiliki kusema mchezo huu ni uhuni, naomba watoe dhana hiyo kwani Jogging zote zinafanya mazoezi ambayo yanasaidia kuondoa magonjwa yasiyoambukiza na kukinga mwili dhidi ya maradhi" Amesema Nkanyenge.
Hata hivyo, amesema kuyakinga magonjwa ni nafuu, kuliko kutibu ugonjwa, hivyo mazoezi yanasaidia kupunguza gharama za matibabu katika kuimarisha afya .
Pia amesema ni lazima kila kikundi cha Jogging kisajiliwe, maana kama hawatasajiliwa kitageuka genge la wahuni lisilofuata Sheria.
Amesema vilabu vikijisajili vikiwa vinalipa ada vitapelekea uhai wa Klabu yenyewe na Chama kwa ujumla.
Amewata Wanajogging wote wahakikishe wanasimamia miradi yao kikamilifu kwani kutokufanya hivyo watajikuta wanapoteza rasilimali Pesa katika mifuko ya wajanja.
Hivyo amewashauri kuchagua viongozi imara wanaowajibika katika kulinda maslahi ya Mwana kikundi katika kufikia malengo yao.
Mbali na hayo, amesema kama mambo yatakwenda sawa watafikiria kuwa na chama cha Kitaifa cha Jogging Tanzania kitakachojali maslahi yao na kuvitambua Vikundi hivyo kwa karibu kama ilivyo michezo mingine.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Jogging Wilaya ya Temeke ( TEJA), Mussa Mtulia, amesema Nyerere alikuwa Namba moja kwenye mchezo wa Jogging, hivyo kitendo cha wao kushiriki kwenye bonanza hilo ilikuwa ni kumuenzi na kuendeleza tasnia hiyo.
Amesema mpaka Sasa katika Wilaya ya Temeke chama chao kimesajili zaidi ya Vikundi 87 na Vikundi 30 vipo kwenye mchakato wa kusajiliwa.
Aidha amesema siku ya leo kwao imetumika katika kuunga mkono Serikali kwa kuutambua michezo huo na kufanya kumbukizi za Baba wa Taifa.
Kuhusu maendeleo ya chama chao, amesema mpaka Sasa tayari baadhi ya Vikundi vimeanzisha vitega uchumi vyao na vingine vinafuata baada ya kupewa sapoti na Manispaa kupitia mfuko wa Vijana.
Katika hatua nyingine, Mwakilishi wa Katibu tawala wa Wilaya ya Temeke ambaye ni msimamuzi wa chama cha Jogging wilayani hapo, Afisa Tarafa Chang'ombe, Aimbora Aminiel Nnko, amewapongeza watu wote walioshiriki katika bonanza hilo huku pongezi kubwa zikiwaendea chama cha Jogging Temeke kwa uwakilishi wao.
Pia amesema Jogging , sio kwa ajili ya Afya, malengo mengine ni kuhamasisha masuala ya kiuchumi katika kuunga mkono Juhudi za Rais John Magufuli katika kufikia Tanzania ya Viwanda na uchumi wa kati.
" Vipo Vikundi vimeweza kukopa na kujiendeleza kiuchumi, hivyo bado Jogging zinanafasi kubwa katika uchumi wetu hususani Tanzania ya Viwanda na uchumi wa kati" Amesema Aimbora.
Hata hivyo , amesema mbali na maendeleo ya uchumi, bado Vikundi hivyo vinachangia damu na kuokoa maisha ya watu wengine. Pia amesema Vikundi hivyo wanavitumia kama njia moja wapo ya kuwapatia majina ya waharifu na kufanya Wilaya ya Temeke kuwa salama.
Katika Bonanza hilo, liliambatana na zoezi la upimaji Afya, Magonjwa mbali mbali kama vile Shingo ya kizazi kwa Wanawake ,Shinikizo la damu n.k.
