TAA yawapiga msasa Wanausalama wake
https://raiatanzania.blogspot.com/2018/05/taa-yawapiga-msasa-wanausalama-wake.html
Na Bahati Mollel, TAA
WANAUSALAMA 18 kutoka Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania
(TAA) wametakiwa kuzingatia mafunzo ya Usalama wa vifurushi na mizigo
vinavyosafirishwa kwa ndege za mizigo yaliyoanza leo kwenye ukumbi wa Chuo cha
Usafiri wa Anga kilichopo kwenye jengo la Kwanza la Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA-TBI).
Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Bw.
Joseph Nyahende, ambapo ameongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia zaidi kuongeza
uelewa wa vifurushi na mizigo hiyo inasafirishwa bila abiria kuambatana nao.
“Tunania njema ya kuwatengeneza wanausalama wetu na hili darasa
ni muhimu sana kwa ajili yenu, hivyo tunahitaji mjifunze kwa faida yenu
binafsi, taasisi na taifa kwa ujumla kwani hamtaweza kuruhusu vitu
visivyostahili kupita kwani mtakuwa sasa mmepata mafunzo ya kuvitambua,”
alisema Bw. Nyahende.
Naye mmoja wa wakufunzi Bw. Sunday Mweemba kutoka Zambia
ameishukuru menejimenti ya TAA ya kuomba kozi hiyo kupitia taasisis ya
Kimataifa ya Usafiri wa Anga (ICAO), ambayo itawafanya wanausalama wake
kutambua vitu vingi vinavyofanyika katika viwanja vingine Duniani.
“Tumeona ni jinsi gani menejimenti yenu ilivyojitoa kwa ajili
yenu, na hii inatolewa na ICAO na kupitia kazi yenu mnatakiwa kuwa makini zaidi
na kuzijua sheria zote zinazohusika na mizigo, na tunamatumaini hadi mwisho
mtakuwa mmeweza kujijengea uwezo,” alisema Bw. Mweemba.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Usalama wa Viwanja vya Ndege
Tanzania, Bw. Julius Misollow alisema mafunzo hayo ni ya kwanza, ambapo
yanalengo la kuwajengea uwezo wanausalama wa kukagua vifurushi na mizigo
inayosafirishwa yenyewe bila abiria kwa kutumia ndege za mizigo.
“Magaidi wamekuwa wakitumia njia mbalimbali na wengine wanatumia
mizigo au vifurushi kufanya hujuma, hivyo tunaimani kwa mafunzo haya
tutawajengea uwezo wa kutambua mizigo ambayo ni hatarishi, ingawa kwa Tanzania
haijawahi kutokea tatizo hilo,” alisema Bw. Misollow.
Hata hivyo, amesema mafunzo hayo yatakuwa na mitihani na
watakaofaulu kwa alama 70 wataendelea na kozi ya ukufunzi ambayo itaanza
baadaye kuanzia Mei 19, 2018.
Washiriki wanaoshiriki na viwanja wanavyotoka ni pamoja na
Philbert Lyimo, Ahmed Zomboko, Thawabu Njeni, Rehema Mlanzi, Nuhu Kisweswe,
Martha Kilunga, Levina Valasa, Josephine Kahimba, Anna Myovela, Fatma Shomari
na Stephen Ntambi (JNIA); Zalia Msangi na Stephen Magambo (Arusha).
Wengine ni Mathias
Gombo, Lilian Malero na Wenceslaus Sango (Mwanza); Bebedict Ole Laput (Songwe);
na Felister Lutonja (Shinyanga).




