https://raiatanzania.blogspot.com/2018/05/mahakama-kuu-divisheni-ya-kazi-yakutana.html
Na Mary Gwera, Mahakama
Mahakama ya Tanzania ipo katika jitihada mbalimbali za
kuhakikika kuwa inamaliza mlundikano wa
mashauri ya Migogoro ya kazi
ikiwa ni pamoja na kufanya majadiliano ya karibu na Wadau wake ili
kukabiliana na changamoto hiyo.
Akifungua Warsha ya siku tatu ya Wadau wa masuala ya Kazi
kujadili juu ya Utatuzi na Usuluhishi wa Migogoro ya Kazi mapema Mei 14, Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Aisha Nyerere alifungua
alisema lengo ni kuwa na uelewa wa pamoja
jinsi ya kutatua migogoro ya kazi.
“Tumewaita Wadau wetu ambao tunafanya nao kazi kwa karibu ili
kuwajengea uwezo kuhusu masuala ya utatuzi na usuluhishi wa migogoro ya kazi
ili wote twende pamoja katika kutatua migogoro hiyo,” alisema Mhe. Jaji
Nyerere.
Jaji Mfawidhi aliendelea kusema kuwa kuna changamoto kadhaa
wanazokabiliana nazo katika uondoshaji wa mashauri ya kazi mojawapo ikitokana
na upande wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) ambapo kuna changamoto ya
rasilimali fedha, rasilimali watu na kadhalika zinazopelekea kuchelewa kwa mashauri
hayo.
Mbali na changamoto hizo kwa upande wa CMA, Mhe. Jaji Nyerere
alibainisha kuwa miongoni mwa sababu zinazopelekea malalamiko ya Mahakama ya
Kazi ni kutokana pia na uchache wa Majaji katika Divisheni hiyo.
Hata hivyo, Mhe. Jaji Nyerere alisema kuwa ili kukabiliana na
upungufu wa Majaji wa Divisheni hiyo, Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania kupitia tamko
la Aprili 30, 2018 ameelekeza kuwa kila Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania
atasikiliza mashauri ya masuala ya kazi.
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
(IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo amesema kuwa katika Warsha hiyo Wadau hao
watafundishwa juu ya Sheria mbalimbali za masuala ya kazi.
“Katika Warsha hii pamoja na Wadau tutapata wasaa wa kuwa na
uelewa wa pamoja juu ya Sheria mpya mbalimbali ikiwa ni pamoja na Sheria ya
Mahusiano kazi ya mwaka 2004,” alieleza Mhe. Kihwelo.
Warsha hii ya Siku tatu inayofanyika katika Kituo cha Mafunzo
kilichopo katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshirikisha baadhi
ya Wadau mbalimbali wakiwemo Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA), Chama cha
Waajiri Tanzania (ATE), Chama cha Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Shirika la
Kazi la Kimataifa (ILO).
Katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano
(2015/2016-2019/2020) Mahakama ya Tanzania imejielekeza kuboresha huduma zake
kupitia ushirikishaji wa Wadau mbalimbali.
Warsha hii imeandaliwa na Mahakama ya Tanzania kwa ushirikiano
na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto chini ya Ufadhili wa Fedha za Mradi wa
Benki ya Dunia.