Jumla ya Waalimu 70 wa Sekondari wahitimu mafunzo ya elimu ya Msingi
https://raiatanzania.blogspot.com/2018/05/jumla-ya-waalimu-70-wa-sekondari.html
MANISPAA ya Ilala imekuwa Manispaa ya kwanza kutoa elimu ya mafunzo ya Waalimu kutoka Shule za Sekondari 70 waliojiunga kufundisha shule za msingi wakidhaminiwa na wakufunzi kutoka Chuo cha Adem , ikiwa ni agizo kutoka Serikali ya kutatua changamoto ya uhaba wa waalimu kwenye shule za msingi.
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo kwenye Shule ya msingi Mnazi Mmoja ambapo mafunzo hayo yalifanyika kwa siku nne, Afisa Elimu Mkoa wa Dar es Salaam, Hamis Lissu, amewapongeza waalimu hao kwa kuitika wito kutoka Serikalini huku akisema haikuwa kazi ndogo kuwapata waalimu hao kwani mpango huo wapo baadhi ya waalimu waliokata tamaa wakijua wanapoteza ajira zao na kushushwa vyeo.

Amesema kuwa, pamoja na mafunzo hayo , bado wapo Waalimu hawakufurahishwa , hivyo amewaambia wasikate tamaa kwani ni ajira kama ilivyo awali, mishara yao na mambo mengine yatabakia kama kawaida.

Aidha, amesema kuwa baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, atalazimika kutembea na kamati yake ili kujua mienendo ya waalimu hao na kujua changamoto wanazokumbana nazo ili kuzitatua.

""Napenda niwaombe ndugu zangu, mimi nishapitia kwenye changamoto nyingi sana, kumbukeni nyie ndiyo mwamvuli wa mafanikio ya Elimu kwa watoto zetu, sasa kama mlikubali kuja huku basi amini kuwa mtanufaika sana na matunda ya kuwa huku, fursa zipo nyingi sana kwa Waalimu wa Shule za Msingi, msikate tamaa pambaneni na mahala penye changamoto msisite kuwakilisha kwa Mkurugenzi ili mpatiwe ufumbuzi haraka hivyo matarajio yangu nikuona kazi mnafanya vizuri kama mlivyokuwa Sekondari""amesema Afisa Elimu Lissu.

Hata hivyo, ametoa maagizo kwa Afisa Elimu wa Manispaa ya Ilala kwamba kazi yoyote itakayotokea Waalimu hao wawe vipaumbele kwani wamefanya maamuzi ya kijasiri na kishujaa.
Amesema kuwa Wafadhili mbali mbali kwa sasa wamekuwa wakileta fedha nyingi kwenye Shule za Msingi ili kusaidia kukuza Elimu , kwa maana hiyo miongoni mwa mambo watakayo nufaika nayo ni pamoja na hizo fursa alizozitaja.Pia amewaomba Waalimu hao kuondokana na hofu ya kushushwa vyeo vyao, lakini msisitizo wake ni kuwajibika kikamilifu kutokana na mafunzo waliyoyapata japo kuna changamoto watakumbana nazo.
Mbali na hayo, amewaomba wakaguzi watakaowakagua Waalimu hao watumie ligha za busara kwani wao ndio kwanza wameingia katika mpango huo, hivyo ni vyema wakawakagua vizuri nasio kwa kuwakemea.
Ameziomba Manispaa zote ambazo zipo nje ya Dar es Salaam, kuiga mfano wa Ilala wakutoa mafunzo hayo kwani wakufunzi wapo vizuri.
Ikumbukwe kwamba, mafunzo hayo yamesimamiwa na Chuo cha Adem chini ya Meneja wa mafunzo ya muda mfupi, Bugendi Joseph, ambapo naye ametoa wito kwa waalimu waliohitimu kuzingatia maadili ya kazi na Elimu waliyoipata kwenye mafunzo hayo.
Naye Afisa Elimu Shule za Msingi Manispaa ya Ilala, Elizabeth Thomas, amesema matarajio yao ilikuwa kupata Waalimu 150, kutokana na changamoto Walimu 70 walijitokeza ambapo waliohudhuria mafunzo hayo mwanzo hadi mwisho ni 65, Waalimu 5 walishindwa kutokana na sababu mbali mbali.

Amewataka Waalimu hao watumie Silaha walizopewa na wakufunzi wao ili kuendeleza gurudumu la Elimu katika shule za msingi.
Miongoni mwa wageni waliohudhuria kwenye kufunga mafunzo hayo ya Waalimu waliokubaliana na mpango wa Serikali kufundisha Shule za Msingi ni pamoja na Meneja mafunzo ya muda mrefu kutoka ADEM, Lucas Mzelela, Afisa Elimu taaluma Manispaa ya Ilala, Rehema Msologonhe, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Msongela Palela ambaye alitoa vyeti kwa wahitimu hao .

Katika hatua nyingine, naye mmoja wa Waalimu waliohitimu mafunzo hayo, Michael Mbata, Mwalimu kutoka Shule ya Sekondari Buyuni, ambaye amepangikatika Shule ya Msingi Bunge, amesema alipatwa mshituko mara ya kwanza lakini baada ya mafunzo hayo amefurahi sana huku akisema Elimu ya Shule ya Msingi ina fursa nyingi sana .
