Miaka 56 ya uhuru CCM Mara yapongeza wanahabari

https://raiatanzania.blogspot.com/2017/12/miaka-56-ya-uhuru-ccm-mara-yapongeza.html
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara, kimewapongeza waandishi wa habari mkoani hapa, kwa kufanya kazi yao ya kuhabarisha jamii kwa weledi mkubwa na kufuata misingi na maadili ya uandishi wa habari, ambapo kimewataka kuendelea na hatua hiyo hasa kipindi hiki ambacho Tanzania bara inatimiza miaka56 ya uhuru.

Katibu wa CCM mkoani Mara, Innocent Nanzaba, alitoa pongezi hizo jana wakati akifunga mkutano mkuu wa waandishi wa habari mkoani hapa, ulifanyika katika ukumbi wa Mativila mjini Musoma.
Nanzaba alisema kuwa waandishi wa habari wote mkoani hapa wamekuwa wakijitahidi sana kutekeleza wajibu wao wa kuandika na kuripoti habari kwa kufuata misingi na maadili ya uandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na kufanya kazi hiyo kwa weledi mkubwa.
Alisema kuwa ni jambo la masingi kwa waandishi wa habari kufanya kazi yao kwa weledi na kwamba CCM mkoani hapa, haina budi kuwapongeza waandishi wa habari wote kwani ni kiungo muhimu na kikubwa kati ya wananchi ya serikali yao.
Aliongeza kuwa Tanzania bara ikiwa inatimiza miaka 56 ya uhuru, pia ni jambo la msingi kwa wana habari, kwani serikali ya awamu ya tano, inayotekeleza Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, kwa ujumla inatambua mchango wa wanahabari na hivyo chama hicho mkoani hapa kitaedelea kushirikiana nao kwani wana wajibu mkubwa kufikisha ujumbe kwa jamii.
Katika hatua nyingine aliwaomba waandishi wa habari kufuatilia kwenye halmashauri za Miji na Wilaya kuangalia kama miradi ya maendeleo zinatekelezwa ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kuibua ubadilifu unaofanywa kwenye halmashauri hizo, sambamba na kwenda maeneo ya vijijini na kuandika habari za kijamii kwani nyingi zimekuwa hazipati fursa ya kuandikwa ili zipatiwe ufumbuzi.
“Waandishi wa habari mko ndani ya Ilani ya CCM, hivyo chama chetu kinatambua mchango wenu katika kusukuma maendeleo, hivyo fuatilieni kwenye halmashauri muwahoji wakurugenzi wanatekeleza vipi Ilani ya uchaguzi kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo” alisema.
Mwenyekiti mpya wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani Mara (MRPC) Robinson Wangaso,aliwataka waandishi wa habari mkoani hapa kushirikiana na kuachana na migogoro isiyokuwana tija, ili klabu hiyo iweze kupata maendeleo endelevu.
Katika mkutano huo ulifanyika uchaguzi wa kuziba mapengo ya nafasi za baadhi ya viongozi akiwemo mwenyekiti wa zamani Jacob Mugini, aliyejiondoa kwenye klabu hiyo ambapo katika uchaguzi huo uliosimamiwa na mjumbe kutoka UTPC Hilda Kileo,wajumbe walimchagua Wangaso kuwa mwenyekiti mpya na makamu wake alichaguliwa Jumanne Ntono, huku mmoja wa wajumbe wa kamati ya utendaji akichaguliwa Hellen Magabe.