Jaji mkuu wa Tanzania awataka Mawakili kulinda taaluma yao kuepukana na rushwa

https://raiatanzania.blogspot.com/2017/12/jaji-mkuu-wa-tanzania-awataka-mawakili.html
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili nchini kutokuwa sehemu ya rushwa
na badala yake waisaidie Mahakama ya Tanzania katika kupambana na rushwa kwa kufanya
kazi kwa bidii na kuzingatia Maadili ya taaluma hiyo.
Akizungumza wakati wa sherehe
za 57 za kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya zilizofanyika leo katika viwanja
vya Karimjee jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu amewataka Mawakili kutokutumia vifungu
vya sheria na kanuni ili kuchelewesha upatikanaji wa haki kwa kuwa suala la
upatikanaji wa haki hutegemea Mawakili.
“Katika karne hii ya 21
ni muhimu kwa Mawakili kufanya kazi kwa bidii kwa kuwa huduma za karne hii huvuka
mipaka ya nchi”, alisema JajiMkuu.
Prof. Juma pia amewashauri
Mawakili kusoma na kuzifahamu sheria za kimataifa ili wawe na upeo mkubwa katika
kushughulikia kesi hasa zile zinazohusisha nchi zaidi ya moja. Baadhi ya kesi hizo
ni zile zinazohusu mipaka ya nchi, makosa ya kimtandao (cyber Crimes) pamoja na
zile zinazohusu Maliasili.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliyataka
baadhi ya makosa ambayo yamekuwa yakifanywa na baadhi ya Mawakili na wananchi kuwashitaki
kuwa ni kutoa siri za wateja, kughushi nyaraka, kutayarisha mikataba zaidi ya moja
kwa lengo la kudanganya, Wakili kuchukua kesi bila ya ruhusa ya mteja, kuwaibia wateja kwa kuwatoza fedha nyingi, kuwadanganya,
kuchukua kesi yenye maslahi binafsi pamoja na uzembe.
Prof. Juma pia amewashauri
Mawakili wapya kuhakikisha wanashirikiana na taaluma nyingine wanapofanya kazi zao
ilikurahisisha na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa wateja wao.
Naye Mwanasheria Mkuu wa
Serikali Mhe. George Masaju amewataka Mawakili wapya kutosubiria kuajiriwa na Serikali
na badala yake wajiajiri na kutoa huduma mikoani na siyo Dar es Salaam peke yake.
Naye Makamu wa Rais wa
Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Wakili Godwin Ngwilimi amewataka Mawakili
nchini kutekeleza wajibu wao kwa kufuata misingi ya haki na kujiepusha na vitendo
vya rushwa.
Jumla ya Mawakili wapya
296 wamekubaliwa na kuapishwa leo na kufanya idadi ya Mawakili nchini kufikia
6,536. Aidha, sherehe za kuapishwa na kukubaliwa kwa Mawakili zimefanyika kwa mara ya 57 tangu kuanzishwa
kwa utaratibu huo mwaka 1986.