Kwandikwa awataka Temesa kuanza mara moja matumizi ya mfumo wa kieletroniki

https://raiatanzania.blogspot.com/2017/11/kwandikwa-awataka-temesa-kuanza-mara.html
NAIBU Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa,
amemtaka Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA), kuanza kufanya
majaribio ya uboreshaji wa mashine za mfumo wa kielektroniki za kukatia tiketi ili kurahisisha
zoezi hilo na kulinda mapato sahihi ya Serikali.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akizungumza
na mmoja wa wafanyakazi mara baada ya kukagua uboreshaji wa mashine za mfumo wa kielektroniki za kukatia
tiketi eneo la Magogoni, jijini Dar es Salaam.
Akikagua huduma zinazotolewa
na vivuko katika maeneo ya Magogoni na Kigamboni jijini Dar es Salaam, Naibu
Waziri Kwandikwa amesisitiza kuwa nia ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanapatiwa
huduma ya usafiri kwa viwango vya kisasa na muda mfupi.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, akipata
maelezo kutoka kwa Mtaalamu wa mambo ya kiufundi kutoka kampuni ya Maxicom
Africa Bw. Peter Mungo, wakati akikagua uboreshaji wa mashine za mfumo wa kielektroniki za kukatia tiketi eneo
la Magogoni, jijini Dar es Salaam.
“Hakikisheni mfumo huu
unaanza kujaribiwa mapema iwezekanavyo ili kama kuna upungufu utakaojitokeza
mkandarasi aushughulikie mara moja kabla ya kipindi cha uangalizi
hakijamalizika”, amesisitiza Mhe. Kwandikwa.
Mtaalamu wa
Vivuko Bernad Daud, akifafanua jambo
kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa, wakati akikagua hali ya
uendeshaji wa vivuko vinavyotoa huduma katika eneo la Magogoni na Kigamboni,
jijini Dar es Salaam.
Ameongeza kuwa
uboreshaji wa mfumo wa kieletroniki wa kukatia tiketi utasaidia kudhibiti
ukusanyaji wa mapato na kutunza kumbukumbu sahihi za abiria wanaopata huduma katika
maeneo hayo.
Naibu Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi) Mhe. Elias Kwandikwa,
akizungumza na baadhi ya abiria wanaopata huduma za vivuko katika eneo la
Magogoni na Kigamboni, wakati alipofanya ziara yake kuona huduma zinavyotolewa
na vivuko hivyo, jijini Dar es Salaam.
Aidha Naibu Waziri
Kwandikwa, amewataka TEMESA kuongeza matangazo ya elimu kwa wananchi ya namna
ya kuchukua tahadhari wanapotumia vivuko hivyo ili kuongeza uelewa na kuepusha
ajali.
Abiria
wakiingia katika Kivuko cha MV Kazi kinachoendelea kutoa huduma za usafiri kati
ya Magogoni na Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Kuhusu huduma
zinazotolewa na vivuko vya Mv. Magogoni, Mv. Kazi na Mv. Kigamboni, mtumiaji wa
vivuko hivyo Bw. Riziki Phillipo, amepongeza juhudi zinazofanywa na Serikali kuhakikisha
usafiri kati ya Magogoni na Kigamboni unakuwepo kwa uhakika na wakati wote.