Meya Kinondoni ataka ukarabati wa kituo cha Afya Kigogo kuharakishwa

https://raiatanzania.blogspot.com/2017/12/meya-kinondoni-ataka-ukarabati-wa-kituo.html
Meya wa Manispaa ya Kinondoni Benjamin Sitta amemuomba mganga mkuu wa manispaa hiyo,kuharakisha ukarabati wa Jengo lililonunuliwa na Serikali kwa ajili ya kituo cha Afya cha Kigogo jijini Dar es Salaam, kukarabatiwa kwa haraka kwa lengo la kusaidia wananchi kupata matibabu kwa haraka ambao utagharimu kiasi cha shilingi milioni 46 .

Akizungumza na wadau mbalimbali waliouzulia katika hafla ya kukabidhiwa hati ya Jengo, sitta amesema eneo hili limenunuliwa na serikali kutoka katika kituo cha Dogodogo Center Street Children Trust(Caring for our Childen) kwa kiasi cha shilingi milioni 400.

Pia sitta amesema mahitaji katika sekta ya afya ni makubwa sana na hivyo serikali inajtahidi kupunguza bajeti kwenye vitu vingine na kuwekeza kwenye sekta ya afya ili wananchi waweze kupata huduma iliyo bora.
"Mahitaji ya wananchi wetu kwenye sekta ya afya bado ni makubwa sana ,lakini kigumu zaidi kwenye manispaa yetu ya Kinondoni tunaufinyu Wa ardhi wakuweza kujenga hospital kubwa Ila kwa kupitia kituo hichi kitaweza kuhudumia wananchi kutoka sehemu mbalimbali.
Aidha amesema katika manispaa hiyo wanategemea kila mtaa uwe na Zahanati na kila Kata kuwe na kituo cha afya ili kufanikisha huduma iliyobora kwa wananchi,pia amesema wanategemea kujenga hospitali ya kisasa maeneo ya Magwepande ikiwa na lengo la kupunguza msongamano katika hospitali ya Mwananyamala,sambamba na kujenga hospitali itakayofanana na huduma za hospitali ya Apolo India ili kuweza kupunguza ongezeko la wagonjwa kwenda kutibiwa nje ya nchi.
"Tumefanya jambo kubwa sana,mategemeo yetu kila Mtaa uwe na Zahanati na kila kata kuwe na Kituo cha Afya, ingawa tuna upungufu wa Zahanati 84, pamoja na vituo vya afya 18 na tumeanza mazungumzo ya kujenga hospitali za kisasa itakayosaidia kupunguza wagonjwa wanaokwenda kutibiwa nje na kuweza kutibiwa hapa hapa " Amesema Sitta.

Kwa upande wake Naibu Meya ambaye pia ni Diwani kata ya kigogo Mangalu Manyama,ameishukuru Serikali katika kufanikisha kununuliwa kwa Jengo hilo ambalo litakarabatiwa na kujengwa kituo cha afya ili kuwasaidia wakazi wa kata ya kigogo kupata matibabu yaliyo bora
Hata hivyo Mganga mkuu wa manispaa ya Kinondoni Dk. Festo Dugange amesema katika halmashauri hiyo inatekeleza Adhima ya serikali ya kujenga Zahanati pamoja na Vitio vya Afya ili kuhakikisha huduma za afya zinaboreka katika jamii ambapo majengo waliyonunua kutoka Dogodogo Center yatasaidia wananchi kupata huduma kwa haraka Zaidi kutoka katika kituo cha Afya kwani Katika Zahanati ya kigogo inahudumia watu 66,654 kutokana na ufinyu wa majengo ya huduma za afya.
”Majengo haya na eneo hili lililonunuliwa kutoka Dogodogo Center itasaidia sana kupunguza msongamano wa Wagonjwa katika Zahanati ya KIgogo kimsingi Zahanati inatakiwa isihudumie wagonjwa zaidi ya 5,000 lakini zahanati yetu inawahudumia wakazi wapatao 66,654 zaidi ya mara kumi na mbili ya uwezo wa zahanati" Amesema Dk. Dugange.

