NEC kufanya Uchaguzi Saranga licha ya tukio la Moto

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imesema kuwa uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Saranga iliyopo Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam utafanyika tarehe 26, Novemba 2017 kama ilivyopangwa, licha ya kuteketea kwa moto vifaa vingi vya uchaguzi baada ya jengo la Ofisi ya Kata hiyo kuungua usiku wa kuamkia jana.
Image result for Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi (NEC) HAMIS MKUNGA
Kaimu Mkurungenzi wa Uchaguzi (NEC) HAMIS MKUNGA amesema hayo jana baada ya kutembelea eneo la tukio na kueleza kuwa tayari ofisi yake imekwishafanya taratibu nyingine ili kuhakikisha kuwa vifaa vyote vya uchaguzi vilivyoteketea kwa moto vinapatikana na kusisitiza kuwa uchaguzi huo utafanyika kama ilivyopangwa.

“Tumefika hapa baada ya kupata taarifa za kuungua kwa jengo la Ofisi ya Kata ya Saranga ambalo pia tulihifadhi vifaa vya uchaguzi mdogo wa udiwani utakaofanyika jumapili ( Novemba 26, 2017) na bahati mbaya vifaa vingi vya uchaguzi vimeteketea vikiwemo rakili, vituturi, fulana na fomu mbalimbali, hata hivyo tayari tumefanya utaratibu wa kuhakikisha vifaa hivyo vinapatikana na uchaguzi unafanyika kama ilivyopangwa awali ”  alisema MKUNGA.

Aidha alieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni hujuma kwani mashuhuda walipofika eneo la tukio walikuta dumu la mafuta ya petroli lakini hawajabaini sababu ya kutokea kwa hujuma hiyo na kuwa vyombo vya ulinzi vinaendelea na uchunguzi zaidi.

Kuhusu hali ya usalama wakati wa uchaguzi MKUNGA alieleza kuwa tayari vyombo vya usalama Wilaya ya Ubungo vimejulishwa na kuwahakikishia wananchi wa eneo hilo kuwa usalama utaimarishwa na kuwataka wajitokeze kwa wingi siku ya kupiga kura.

MKUNGA alisema kuwa bado hawajaweza kubaini kiwango halisi cha hasara kilichopatikana na kutokana na ajali hiyo na kuwa ofisi yake inaendelea kufanya tathmini juu ya hasara hiyo.
   
Naye Mkuu wa Idara ya Uchaguzi NEC,  IRENE KADUSHI amesema kuwa, kata ya Saranga ina vituo vya kupigia kura 139 ambapo vifaa vyote vya uchaguzi awamu ya kwanza na ya pili vilikuwa vimekwishafika na kuwa awamu ya mwisho ya usafirishaji wa vifaa vya uchaguzi katika kata hiyo ilikuwa ni jana asubuhi lakini walilazimika kuzuia upelekaji wa vifaa hivyo kutokana na tatizo hilo.

Aidha alisema kuwa shughuli zote za uchaguzi ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uchaguzi zimehamishiwa katika Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo kwa usalama zaidi, na kusisitiza kuwa taratibu nyingine zinaendelea na uchaguzi huo utafanyika kama ulivyopangwa.

Related

habari 8322482987077343306

Post a Comment

emo-but-icon

item